Friday 28 April 2023

MKUU WA WILAYA YA TANGANYIKA AWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA AFYA BULAMATA.



Muonekano wa Jengo la OPD Kituo cha Afya Bulamata.

MKUU wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu Aprili 25,2023 alitembelea na kukagua mradi wa kituo cha Afya Bulamata kisha kuweka jiwe la msingi.

Kituo cha Afya Bulamata awali kilipokea shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la nje (OPD), maabara na kichomea taka kabla ya kuongezewa tena shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kufulia, jengo la upasuaji na jengo la Mama na mtoto pamoja na ujenzi wa njia.

Mradi ulianza kujengwa mwezi Desemba 2021 na hadi sasa umekamilika na umeenza kutoa huduma kwa wananchi wa Kata hiyo na maeneo jirani.

Aidha, mara baada ya kuweka jiwe la msingi mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu alizindua zoezi la ugawaji vyandarua bure kwa mama wajawazito waliofika kupata huduma katika kituo hicho.

"Leo tunawapa vyandarua tunaomba mkavitumie kujikinga na Malaria. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hataki kuona mwananchi wake anapoteza maisha kwa sababu ya Malaria ndiyo maana ameleta vyandarua na Madaktari"

Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu (kulia) akifuarahi na Diwani wa Kata ya Bulamata baada ya kuweka Jiwe la Msingi kituo cha Afya Bulamata.

Mkuu wa wilaya akimkabidhi chandarua mama mjamzito kama sehemu ya Serikali kuwakinga Wananchi wake dhidi ya Malaria.

Awali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Tanganyika, Dkt. Alex Mrema alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa Serikali imeleta vifaa kwa ajili ya mama wajawazito ikiwemo vyandarua ambavyo vitakawiwa bure.

Baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma katika kituo hicho wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea kituo cha Afya karibu kwani mwanzo walikuwa napata shida kufuata huduma maeneo ya mbali.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment