Wednesday 16 August 2023

WILAYA YA TANGANYIKA IKO TAYARI KUUPOKEA MWENGE WA UHURU AGOSTI 24,2023.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu akizungumza na Wanahabari Ofisini kwake.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu amesema Serikali wilayani humo na Wananchi kwa ujumla wamejiandaa na wapo tayari kuupokea Mwenge wa Uhuru utakao wasili wilayani humo Agosti 24 mwaka huu na kupokelewa eneo la Kijiji cha Vikonge ukitokea mkoani Kigoma kabla ya kukabidhiwa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Agosti 25,2023.

DC Buswelu ameyasema hayo Jana Agosti 15, 2023 wakati akizungumza na Wanahabari Ofisini kwake eneo la Mpanda ndogo, Ifukutwa.

Amesema Mwenge wa Uhuru baada ya kupokelewa utafanya mkesha Kasekese kabla ya kukimbizwa kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali.

Aidha, Mhe. Buswelu ameitaja miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru kuwa ni pamoja na uzinduzi wa mradi wa maji uliopo Kijiji cha Vikonge uliogharimu kiasi cha zaidi ya Tsh. milioni Mia sita na nane, pia Mwenge utatembelea Klabu za Lishe, Klabu za kupinga na kupambana na rushwa sambamba na kutembelea miradi upandaji miti pamoja na kutembelea kikundi cha Vijana ambao wananufaika na mkopo wa Halmashauri.

Mhe. Buswelu ameongeza kuwa, miradi mingine ni pamoja na kutembelea na kuzindua jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Kituo cha Afya Sibwesa, kuzindua Shule mpya ya msingi Kasekese, kutembelea na kukagua barabara inayounganisha Kagunga na Kasekese iliyokarabatiwa kwa kiasi cha Tsh. milioni 300.

"Eneo lingine ambalo Mwenge wa Uhuru utatembelea ni kwenye ujenzi wa Zahanati ya Kagunga. Mradi huu ni mradi ambao umetekelezwa kwa fedha ambazo zinatokana na mapato ya hewa ukaa ambayo inatokana na utunzaji wa mazingira"- Aliongeza DC Buswelu.

Kadhalika, Mkuu huyo wa Wilaya amesema baada ya kutembelea mradi wa Zahanati hiyo litafuata zoezi la upandaji miti katika viunga vya Zahanati hiyo ikiwa ni ishara ya Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mapambano ya kulinda na kutunza maliasili.

Hata hivyo, amesema miradi yote ambayo itatembelewa na Mbio za Mwenge wa Uhuru inagharimu kiasi cha takribani bilioni 1.9

Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inasema "Tunza Mzingira, Okoa vyanzo vya maji kwa Ustawi wa Viumbe hai kwa Uchumi wa Taifa"

Baadhi ya Viongozi waliohudhuria kikao cha DC na Wanahabari.

No comments:

Post a Comment