Friday 28 April 2023

WANANCHI TANGANYIKA WAADHIMISHA MUUNGANO KWA KUIISHUKURU SERIKALI.

Msafara wa viongozi mbalimbali wakiongozwa na mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu ukiwa eneo la mradi wa daraja linalojengwa katika mradi wa ujenzi barabara ya Vikonge - Luhafwe (km 25). Aprili 25,2023

WANANCHI wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi wameadhimisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Vikonge hadi Uvinza mkoani Kigoma kwa kiwango cha lami.

Wakizungumza mbele ya msafara wa mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu aliyeambatana na viongozi wengine walipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Vikonge - Luhafwe (km 25) Aprili 25,2023 walisema kabla ya Uhuru walilazimika kukatiza maporini kufuata huduma za Afya jambo lililosababisha vifo kwa Mama wajawazito.

"Tulipata shida sana, unakuta mama mjamzito anatoka mbali wanapopatwa na uchungu mtu anazalia njiani, kiti (mtoto) kinakataa kutoka mtu anafariki" Alisema Devotha Titto mkazi wa Kijiji cha Vikonge.

Alisema mbali na kuwarahisishia usafiri lakini pia anaimani hata kiwango cha nauli kitakuwa chini ikiwemo ufupi wa safari kutoka Mpanda hadi Kigoma kwani kwa sasa wanatumia hadi masaa Sita kufika mkoani Kigoma.

Diwani wa Kata ya Tongwe Frank Kidigasi alisema kukamilika kwa barabara hiyo ya Mpanda - Kigoma itafungua fursa kwa wakazi wa Tanganyika na Katavi kwa ujumla kufanya biashara Kigoma na nchi jirani za Congo, Rwanda na Burundi kwa kuuza mazao yao kwa kuwa mkoa wa Katavi ni wa Kilimo.

Diwani wa Kata ya Tongwe Frank Kidigasi

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji mradi huo, Kaimu Meneja Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Katavi Mhanfisi Emily Zengo alisema barabara hiyo inajengwa kwa fedha za ndani kwa ghalama ya Tsh. bilioni 35.638.

Alisema, kazi inayofanyika ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kukata sehemu ambazo milima iko juu sana, ujenzi wa daraja kubwa Mnyamasi lenye urefu wa mita 61.8 na kina cha mita 5 ambalo litakuwa suluhisho eneo hilo kwa kuwa mvua zinaponyesha maji yanapita juu ya barabara.

Kaimu Meneja Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Katavi Mhanfisi Emily Zengo.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu alisema ziara hiyo ni kuadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo amemhakikishia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Serikali ya Tanganyika itasimamia miradi yote kwa ufanisi ili Wananchi waweze kupata thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu akifurahia na Wananchi baada ya kutembelea mradi wa barabara katika maadhimisho ya sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment