Friday 26 May 2023

DC BUSWELU AHIMIZA UKWELI KWENYE MAENDELEO AMBAYO SERIKALI INAYAFANYA

MKUU wa wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu

Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Tanganyika, ACP Kiberiti

MKUU wa wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu ametoa wito kwa watanzania kuwa wakweli katika maendeleo ambayo Serikali inayafanya pasipo kupotosha.

DC Buswelu ametoa wito huo baada ya kutembelea na kukagua hatua ya ujenzi wa kituo cha Polisi Tanganyika, ambapo amsema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya Askari Polisi wilayani humo ikiwemo kuwajengea nyumba Watumishi wa Jeshi hilo.

Hayo yamejiri baada ya kauli ya Katibu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Salumu Mwalimu akiwa ziarani wilayani humo kutoa kauli ambayo siyo ya kweli kuwa OCD hana nyumba ya kuishi wakati viongozi wengine wamejengewa nyumba na Serikali.

"kuna nyumba kubwa imeshakamilika three in one. Polisi hawajasahaulika na kazi inaendelea vizuri wapo ambao tayari wameshahamia kwenye nyumba zile, nyumba zina maji na umeme"

Nyumba ya watumishi wa Jeshi la Polisi (Three in One)

Aidha, DC Buswelu amesema licha ya kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo, Serikali inajenga kituo cha kisasa cha Polisi kitakacho ghalimu shilingi milioni 500 ambapo ujenzi wake umefikia hatua ya kumwaga jamvi.

Kwa upande wake Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Tanganyika, ACP Kiberiti amesema kwa kiasi kikubwa uwepo wa nyumba hizo umesaidia wananchi kupata huduma ya kiusalama haraka.

ACP Kiberiti ameongeza kuwa, ujenzi wa kituo cha  Polisi ulisimama kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha kutokana na jeografia ya wilaya hiyo hivyo ujenzi utaendelea hivi karibuni.

MWISHO.

Monday 15 May 2023

DC TANGANYIKA AWATAKA WAZAZI KUTENGA MUDA WA KUZUNGUMZA NA WATOTO WAO.



MKUU wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu ametoa wito kwa wazazi kurudi enzi za nyuma kwa kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao mara kwa mara badala ya kuwawekea katuni kwenye runinga huku watoto wakiendelea kuharibika kimaadili.

DC Buswelu ametoa wito huo leo Mei 15,2023 katika maadhimisho ya Siku ya Familia duniani yaliyofanyika Kiwilaya katika viwanja vya Shule ya Msingi Ifukutwa, Halmashauri ya Tanganyika Mkoani Katavi.

Amesema yapo mambo yanafanywa na jamii yasiyompendeza Mungu kama mapenzi ya jinsia moja na vikiwemo vitendo vya ukatili, ukichunguza vinatokana na kukosekana kwa maadili  hivyo ipo haja ya wazazi na walezi kuwatengenezea misingi mizuri watoto wao kabla hawajaharibika.

Akilejea maneno ya Mungu katika Biblia, DC Buswelu amesema Mungu alipoona matendo maovu yamekithiri katika uso wa dunia, alichukia na kushusha gharika na sodoma na gomola ikateketea na watu wote, na ameitaka jamii kuachana na matendo maovu kabla Mungu hajachukia na kushusha gharika.

"Ili haya yatuepuke lazima turejee kwenye kuwekeza kwenye Utu, tuwekeze kwenye Ubinaadamu, tuwekeze kwenye Upendo, tuwekeze kwenye Umoja, tuyajenge maadili ya Taifa letu kuanzia ngazi ya Familia"

Mzee maarufu, Hassan Mapengo mkazi wa Tanganyika amesema zamani wazazi walikuwa na utamaduni wa kukutana na watoto wao ndiyo maana hapakuwa na matendo ya unyang'anyi, kuporomoka kwa maadili tofauti na sasa ambapo wazazi hawana muda wa kuzungumza na watoto zaidi wanarudi usiku.

MWISHO.

Monday 8 May 2023

WILAYA YA TANGANYIKA: YAWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KWA AJILI YA KILIMO NA MIFUGO.





HAYO yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mheshimiwa Onesmo Buswelu alipoitembelea kampuni ya Meru Agro Wilayani Mbozi akiwa pamoja na kamati ya ulinzi ya Wilaya, Waheshimiwa Madiwani na Wakuu wa Idara.

Ziara hiyo ilifanyika Tarehe 05/05/2023 hadi Tarehe 7 ikiwa ni kuitembelea kampuni ya Meru Agro kuona namna inavyozalisha mbegu Mbalimbali, viuatilifu na vifaa vya shambani.

Mheshimiwa Buswelu alisema "Nawaomba Muje muwekeza Tanganyika, ardhi ipo ya kutosha, usalama upo na wataalam wa kufanya nao kazi wapo". Pia alisisitiza kufanya tafiti za udongo katika eneo la Wilaya hiyo ili kujua ni mbegu zipi zinafaa kutumika katika eneo hilo.

Kwa upande wake Christopher Shimwela, Meneja wa kampuni ya Meru Agro kanda ya Mbeya, alisema msimu uliopita walizalisha mbegu tani elfu tano na zote ziliisha. "Na Msimu huu tunategemea kuzalisha tani zaidi ya elfu sita"

Pia Mkurugenzi wa Meru Agro Ndugu Matanga Chacha alisema "Tupo tayari kuwekeza Tanganyika na tumeagiza mitambo ya thamani ya Shilingi Billioni 2 itakayotumika katika kilimo Wilayani Tanganyika" pia aliomba apewe ekari elfu tano kwa ajili ya uwekezaji huo.

Shabani Juma Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika alimuhakikishia muwekezaji huyo kutoa eneo la ekari elfu tano kama atafuata vigezo vilivyowekwa na Wilaya hiyo pamoja na kamati ya uwekezaji.

Pia msafara wa Mkuu wa Wilaya na Madiwani pamoja na wakuu wa Idara ulipata nafasi ya kutembelea Shamba la Mahindi lenye ekari elfu tatu lililopandwa mahindi aina ya Meru HB 515, Meru HB 513, Meru HB 405 na Meru HB 623 pamoja na mbegu za mahindi ya asili aina ya Situka M1.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Ahmed Mapengo alimtaka muwekezaji huyo kuwa na nia ya dhati kuwekeza katika eneo hilo. "kumekuwa na watu wengi wababaishaji na hawana nia ya kufanya uwekezaji, wanapewa maeneo na wanayatelekeza" Alisema

Wilaya ya Tanganyika imetenga eneo la Luhafwe lenye Hekta 46 elfu kwa ajili ya uwekezaji wa miundombinu ya Kilimo na Mifugo.

MWISHO.