Tuesday 28 March 2023

TANGANYIKA: VIONGOZI WA KATA NA VIJIJI WAPEWA SEMINA YA USIMAMIZI WA MIRADI YA HEWA UKAA.

Baadhi ya Watendaji wakifatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo katika utekelezaji na usimamizi wa miradi ya Hewa Ukaa yanayofanyika katika Ukumbi wa Mkurugenzi jengo la Halmashauri Machi 27,2023


VIONGOZI wa kata na vijiji vinavyonufaika na mradi wa hewa ukaa katika Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi leo wameanza mafunzo ya siku tatu yatakayohusisha mada mbalimbali ikiwemo dhana ya utawala bora na utunzaji wa nyaraka.

Akizungumzia yatakayojadiliwa katika mafunzo hayo Mratibu wa miradi ya hewa ukaa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Alfonce Mwakyusa amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa kata na vijiji pamoja na Wenyeviti wa vijiji ili kuimarisha usimamizi utakaozingatia utawala bora, namna ya kuibua miradi hiyo na matumizi sahihi ya fedha zitokanazo na mauzo ya hewa ukaa.

Ameongeza kuwa, fedha zinazotokelewa ni nyingi ambapo katika awamu hii ya Sita na Saba vijiji nane vinavyo nufaika na mradi wa hewa ukaa vimeingiziwa Tsh. Bilioni 4.27 hivyo kutakuwa na mada kuhusu uhandisi ujenzi na mada kuhusu masuala ya rushwa.

Bw. Alfonce Mwakyusa Mratibu wa miradi ya hewa ukaa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Akifungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Ukumbi wa Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewataka washiriki kuwa kutilia maanani mafunzo hayo kwani serikali haitataka kusikia Kijiji chochote kikienda kinyume au kuharibu mradi ikwemo udanganyifu katika kupata wazabuni.

"Yaani Vijiji vyoye 55 vifeli kuna Wilaya hapo? Wewe kwenye eneo lako unapotengeneza mikakati ya kufelisha maana yake unataka nchi yote ifeli. Unapotengeneza mikakati ya kuiba hata senti moja maana yake unataka nchi yote ifeli halafu mwisho wa siku tukimbile wapi? Mimi nawasihii, msifanye hivyo" 

Kataika hatua nyingine, DC Buswelu ameagiza kufikia Aprili mosi mwaka huu Vijiji vyote vunavyo nufaika na mradi viwe vimeingiziwa fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi.

Mhe. Onesmo Buswelu,Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika na mgeni rasmi katika mafunzo hayo akifafanua jambo.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wamesema wanaamini kupitia mada zinazowasilishwa wataenda kusimamia ipasavyo fedha na utunzaji sahihi wa nyaraka, usimamizi mzuri wa miradi kwani awali walikuwa hawana weledi na masuala hayo.



MWISHO.

Thursday 23 March 2023

SERIKALI YATENGA BILIONI 9 KUANZISHA KILIMO CHA UMWAGILIAJI KATIKA MASHAMBA YA MPUNGA YA GEREZA LA KALILANKULUKULU TANGANYIKA.


SERIKALI ya Tanzania imetenga kiasi cha Tsh. bilioni 9 kwa ajili ya kuanzisha Kilimo cha umwagiliaji katika mashamba ya mpunga ya Gereza la Kalilankulukulu katika Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Akizungumza baada ya kutembelea wakulima mbalimbali Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesema hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu kiasi cha Tsh. Milioni mia nane kitakuwa kimeshaingizwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji katika eneo hilo lenye ukubwa wa takribani Ekari mia tano.

DC Buswelu amemhakikishia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa watahakikisha wanasimamia kikamilifu na kwa ukaribu mradi huo kwa kuwa si tu utawanufaisha Magereza bali utanufaisha pia wananchi wa mkoa wa Katavi na Taifa kwa ujumla.
Onesmo Buswelu Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza hilo, SP Bosco Paulo Lupala amesema katika msimu huu wa Kilimo wamelima Ekari 150 za zao la mpunga kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa ambapo wanatarajia kuvuna gunia 1700 mpaka 2000 sawa na Tani mbili za mpunga.

SP Lupala amemshukuru Rais kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuliendeleza eneo hilo kwani ujio wa mradi huo utawapunguzia changamoto mbalimbali huku wakitarajia uzalishaji kuwa mkubwa zaidi kutokana na zana za kisasa zitakazotumika ukilinganisha na ukubwa wa eneo.
SP Bosco Paulo Lupala, Mkuu wa Gereza hilo la Kalilankulukulu.

Nae Afisa Kilimo Wilaya ya Tanganyika Philemon Mwita amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili watumie kanuni bora za Kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya pembejeo.

Kufuatia mradi huo mkubwa, baadhi ya wananchi wawanaozunguka eneo hilo wamemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwakumbuka na wanaamini ni mradi utakaowanufaisha ikiwemo kukabiliana na changamoto ya mvua.

Machi 22,2023 Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika akiwa ameambatana na Afisa Kilimo wametembelea wakulima wa mazao mbalimbali ikiwa ni kujionea hali ilivyo baada ya mbolea ya ruzuku iliyotelewa na Serikali kama ilitumika ipasavyo na wamejirisha uzalishaji utakuwa mkubwa kutokana na wakulima kuitumia fursa ya pembejeo ya ruzuku.






Thursday 9 March 2023

SERIKALI KATAVI KUENDELEA KUIMARISHA UWEZESHAJI WANAWAKE.

MKUU wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema serikali itaendelea kutoa uwezeshaji kwa wanawake kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wanawake kushiriki katika biashara na uzalishaji.

Akihutubia katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani Machi 8, 2023 yaliyoadhimishwa kimkoa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mpanda Ndogo wilayani Tanganyika, Mrindoko amesema licha ya mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa wanawake, serikali itaendelea kuimarisha maeneo ya biashara yatayowavutia wanawake.

Aidha amewasisitiza wanawake kujielimisha katika kutambua haki zao ikiwemo haki ya kumiliki mali hasa ardhi, haki ya kupata elimu na usawa katika kufanya kazi.





Awali akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi Afisa maendeleo Msaidizi wa mkoa wa Katavi, Kennedy Wilson amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita halmashauri za mkoa huo zimetoa mikopo kwa vikundi vya wanawake yenye jumla ya shilingi bilioni 1.5 

Aidha amesema katika mwaka wa fedha unaoendelea wa 2022/23 Halmashauri za mkoa wa Katavi tayari zimeshatoa mikopo yenye jumla ya shilingi 339.3 kwa vikundi 49 vya wanawake. 

Wilson amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao wa 2023/24 halmashauri za mkoa wa Katavi zinatarajia kutoa mikopo inayofikia shilingi milioni 547.9 kwa vikundi mbalimbali vya wanawake mkoani humo.

Afisa maendeleo Msaidizi wa mkoa wa Katavi, Kennedy Wilson.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mrindoko amesema Serikali mkoani Katavi haitasita kumchukulia hatua mwajiri yeyote atakayebainika kutoa ajira kwa kumbagua Mwanamke kutokana na jinsia yake.

''Kama kutakuwa na mwajiri yeyote ambaye atatoa haki kwa kubagua Mwanamke sio kwa karne tuliyonayo sasahivi, hatutamvumilia mwajiri yeyote ambaye atakosesha haki ya mtumishi Mwanamke kwa kumbagua kwa sababu yeye ni Mwanamke'' Alisema RC Mrindoko.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka huu yamepambwa na kaulimbiu inayosema  "UBUNIFU WA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA: CHACHU KATIKA KULETA USAWA WA KIJINSIA"

MWISHO.

Wednesday 8 March 2023

KATAVI: CHUO CHA VETA KUJENGWA WILAYANI TANGANYIKA, EKARI 20 ZATENGWA.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi imetoa ekari 20 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilayani Tanganyika.

Akizungumza walipokwenda kulitembelea eneo hilo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Shaban Juma amesema kama Halmashauri imejipanga kuhakikisha chuo hicho kinajengewa.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Shaban Juma.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesema watahakikisha wanasimamia ujenzi kwa kuwa kuna Vijana wengi ambao walio hitimu darasa la saba na kidato cha nne hivyo kukamilika kwa chuo hicho itakuwa mkombozi kwa Vijana wengi wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Magharibi, Shomari Omary amesema wameamua kujenga chuo hicho Tanganyika baada ya kugundua kuna uhitaji mkubwa.

Omary amesema wameridhishwa na mandhari ya eneo hilo na mikakati ya ujenzi itaanza mwishoni mwa mwezi huu endapo watapata hati miliki ya eneo hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Magharibi, Shomari Omary.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tanganyika Hamad Mapengo ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA).

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tanganyika Hamad Mapengo.

MWISHO.

Tuesday 7 March 2023

KATAVI: RC MRINDOKO AWAJULIA HALI MAJERUHI 30 WA AJALI ILIYOUA WATU 9.


WATU 09 wamefariki dunia na wengine 30 kujeruhiwa kutokana na ajali mbaya iliyotokea mlima mkali wa Nkondwe, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi baada ya basi aina ya Tata lenye namba za usajili T506 DHH kampuni ya Komba's kupinduka na kudondokea korongoni.

Taarifa ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Dkt. Alex Mrema imesema vifo hivyo tisa vimetokea papo hapo ambapo kati ya waliofariki wanaume ni 5 kati yao watu wazima ni 2 na watoto 3 na huku wanawake wanne wakipoteza maisha katika ajali hiyo akiwemo mjamzito.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Dkt. Alex Mrema akitoa taarifa ya Ajali kwa Mkuu wa Mkoa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi Ali Makame amesema ajali hiyo imetokea Machi 6, 2023 alasiri majira ya saa Tisa dakika 45 baada ya kufika katika mlima huo gari liliserereka na kudondokea kwenye korongo kubwa lenye kina cha mita zisizopungua 75.

Amesema hadi sasa chanzo cha ajali hakijajulikana na Jeshi la Polisi mkoani humo wanaendelea na uchunguzi huku zoezi la kuitambua miili likiendela kwa ajili ya taratibu zingine.


Picha mbalimbali za muonekano wa ajali ilivyo.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akiwa hospitali ya wilaya ya Tanganyika kuwajulia hali majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu, amesema kama Serikali imeguswa kwa ajali hiyo huku akitoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waliopoteza maisha kwani Taifa limepoteza nguvu kazi.

Aidha,amewapongeza viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika, wataalamu wa afya na Wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza haraka kusaidia kuwaokoa wale waliopata ajali.

"Kuna baadhi walikuja wakiwa na hali si nzuri lakini mara baada ya kupata huduma za afya hapa hospitali ya wilaya ya Tanganyika tayari hali zao zimeendelea kuimarika, tuendelee kuwaombea waliopata majeraha waweze kupona haraka"
Mhe. Mwanamvua Mrindoko, Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

Moja ya majeruhi katika ajali hiyo Philbert Focus, mkazi wa Mpanda amesema wakati wamefika katika mlima huo ghafla kwenye kona gari lilienda kwa kasi kubwa kama limekatika breki ndipo lilipomshinda dereva na kuoitiliza kwenye korongo.

"Niliona kama giza baadae nikawa nimefumbua macho nikajikuta naumia nipo ndani gari limelala juu chini nikajikwamua kutoka japo kulikwa na kanafasi kadogo. Maumivu niliyopata ni ya mkono na michubuko kichwani na mguuni"
Philbert Focus, Majeruhi

Naye Hamadi Kambi shuhuda wa ajali hiyo amesema katika harakati za kushirikiana na Jeshi la Polisi kuokoa majeruhi, anasema ajali ilikuwa mbaya sana na katika kuokoa watu wanne wamefia mikononi mwake.

"Kuna mtoto mama yake kanifia mikononi, yule mtoto kanisikitisha sana"

Akiongea kwa niaba ya Wananchi, Mwenyekiti wa mtaa wa Luhafwe Raphael Lutonja amesema eneo hilo ni baya sana na mara kadhaa kumekuwa kukitokea ajali na kusababisha vifo huku akidai ajali iliyotokea leo ni mbaya zaidi kuliko ajali ambazo zimewahi kutokea eneo hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amewashukuru wanacnhi kwa kusaidiana na Serikali katika zoezi la uokoaji ikiwemo kujitolea vyombo vya usafiri kwa ajili ya kuwakimbiza majeruhi Hospitali.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu.

MWISHO.

Saturday 4 March 2023

WANANCHI WA MISHAMO WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUANZA UTEKELEZAJI MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI.


WANANCHI wilayani Tanganyika mkoa wa Katavi wameipongeza Serikali kwa hatua ya kuanza utekelezaji wa upimaji wa matumizi bora ya Ardhi kwani itasaidia kuleta amani na utulivu ikiwemo kuondoa migogoro hasa ya wakulima na wafugaji.

Pongezi hizo wamezitoa wakati timu ya wataalamu wa Ardhi mkoa wa Katavi wakiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ilipofika na kuzungumza na Wananchi wa kata ya Mishamo halamshauri ya wilaya ya Tanganyika juu ya mpango wa Serikali kutekeleza mpango huo.

"Nimefarijika na wenzangu na ujio wenu kuja kutuwekea huu utaratibu, bila shaka itaepusha mambo mengine ambayo yalikwa yanatukosesha amani na utulivu kwa kuwa mtakuja kutenga sehemu ya kilimo, sehemu za ufugaji watu wote tutaishi kwa amani na utulivu" Amesema Ndayegamiye Seth, mkazi wa Mishamo.
Ndayegamiye Seth, mkazi wa Mishamo.

Kwa upande wake Ibrahim Butta, Afisa mipango miji Mkoa wa Katavi amesema mpango wa matumizi bora ya Ardhi una manufaa kwa wananchi kwa kuwa Serikali hupeleka miradi sehemu nyenye mpangilio mzuri wa Ardhi kwa kuwa pia ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wanaishi katika mpangilio unaoeleweka.

Amesema mpango huo unasimamiwa na Wananchi wenyewe wakiwaongoza wataalamu kwa kuwa wao ndio wenye kuijua mipaka na kupendekeza matumizi ya Ardhi katika eneo lao na amewaomba wananchi kutoa ushirikiano pale wataalamu watakapopita kutoa elimu na kupata taarifa mbalimbali.
Afisa mipango miji Mkoa wa Katavi, Ibrahim Butta.

Nae Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwa suala la mipango bora ya Ardhi ndio ufunguo wa maendeleo Duniani kote kwani bila mpango huo migogoro itaendelea kuwepo na kusababisha kukwamisha maendeleo.

Ametoa wito kuwa makundi yote yashirikishwe katika zoezi zima la upangaji huku akiwaonya wote watakaobainika kuhujumu mpango huo.
Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu.

Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Nehemia James amesema kutokana na umuhimu wa zoezi hilo tayari Serikali ya mkoa imepata baraka kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na utekelezaji wake utafanyika eneo la makazi ya wakimbizi ya Mishamo na Katumba.






MWISHO.

Thursday 2 March 2023

KAMPENI YA 'SHINDA MALARIA' YAZINDULIWA MKOANI KATAVI.

MKUU wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko Jana Machi 01, 2023 amezindua kampeni ya 'SHINDA MALARIA' inayotekelezwa katika Halmashauri mbili za Tanganyika na Nsimbo yenye lengo la kupunguza maambukizi, vifo na madhara ya kuugua Malaria hasa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na mama wajawazito.


Mradi wa 'SHINDA MALARIA' unatekelezwa na Taasisi ya afya ya Ifakara kwa ufadhili wa USAID|PMI.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, Mkurugenzi mkuu wa mradi wa 'SHINDA MALARIA' kutoka taasisi ya afya ya Ifakara Dkt. Dunstan Bishanga, amesema Mkoa wa Katavi ni kati ya mikoa Saba ambayo Wizara ya Afya imeitambua kama mikoa yenye maambukizi ya hali ya juu ya Malaria.

Amesema katika utafiti wa mwaka 2022 kwenye ngazi ya jamii ya ukubwa wa tatizo la Malaria ilikadiriwa watu 8 kati ya 100 mkoani Katavi wana vimelea vya Malaria.

Amesema katika kuhakikisha mapambano dhidi ya Malaria yanafanyika afua mbalimbali zinafanyika katika vituo vya Afya na ngazi ya jamii kwa kutoa huduma ya mkoba katika maeneo ambayo ni ngumu kufikika kwa kushirikiana na timu za uendeshaji na usimamizi wa afya za Mkoa na Halmashauri husika.

Dkt. Bishanga amesema katika kipindi cha miezi 7 mradi umetoa mafunzo kwa watoa huduma 36 watakaoweza kutoa huduma za Malaria ngazi ya jamii na watoa huduma waelimishaji 58 ikiwemo kuwapatia vitendea kazi.

"Umuhimu wa huduma hizi umejidhihirisha kwamba kati ya watu waliohudhuria hapa leo wameshapimwa mpaka sasa huduma zinaendelea watu takribani 100 na kati ya hao watu 3 kati ya watu 10 wamekutwa na vimelea vya Malaria, watu 3 kati ya 10 ni wengi sana katika takwimu za kawaida"
Mkurugenzi mkuu wa mradi wa 'SHINDA MALARIA' kutoka taasisi ya afya ya Ifakara Dkt. Dunstan Bishanga.

Nae mwakilishi wa USAID|PMI Lulu Msangi amesema toka mwaka 2020 PMI kwa kushirikiana na Serikali imesaidia uimarishaji wa ubora wa vituo vya Afya katika kutoa huduma bora za afya ambapo juhudi hizo zimepunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini kutoka asilimia 18 mwaka 2015 mpaka asilimia 8 mwaka 2020.

Aidha, ili kuendelea kupunguza ugonjwa wa Malaria mkoani Katavi PMI imetoa msaada wa vitendelea kazi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambavyo ni Baiskeli 21, Mikoba ya kuwekea vifaa 21, vipima joto 21, mizani ya kupimia uzito ya mgonjwa 21, masanduku 21 yaliyo na vifaa vya afya zikiwemo simu za mkononi 36 kwa ajili ya watendaji wa afya ngazi ya jamii na simu 26 za ziada vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 47.5

Lulu Msangi, mwakilishi wa USAID|PMI.

Kwa upande wake mgeni rasmi amepongeza na kushukuru wadau wote walioshiriki kuleta mradi huo katika Mkoa wa Katavi kwa kuwa ugonjwa wa Malaria ni kati ya tatizo linaloikabili nchi na katika kulinda heshima ya mradi huo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria ametoa wito kwa watoa huduma kuwa waadilifu katika kuwahudumia wananchi na atakaye bainika kwenda kinyume ikiwemo kutumia vibaya vifaa vilivyokabidhiwa atachukuliwa hatua za kisheria.

Pia amewataka wananchi kuacha imani potofu hasa kwa magonjwa ya mripuko ikiwemo Surua na kipindupindu badala yake wafike kwenye vituo vya Afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu ikiwemo chanjo mbalimbali za magonjwa ikiwemo chanjo ya Malaria, Surua na maradhi mengine.

Mrindoko amewaomba wafadhili wa mradi wa 'SHINDA MALARIA' kupanua wigo ili huduma hiyo itolewe katika Halmashauri zote tano za Mkoa huo.

Mradi huo unaofadhiliwa na USAID|PMI na kutekelezwa na Taasisi ya afya ya Ifakara ulianza kutekelezwa agosti 2022 na unatekelezwa kwa ufanisi katika Mkoa wa Katavi pekee Tanzania nzima kwa muda wa miaka mitano katika Halmashauri hizo mbili.



PICHA mbalimbali zikionyesha vifaa vilivyokabidhiwa na Mgeni rasmi.






MWISHO.