Friday 28 April 2023

TANGANYIKA MUUNGANO CUP YATAMATIKA KWA MAJALILA FC KUIBUKA MSHINDI.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu akimkabidhi kikombe kepteni wa Majalila FC Naseeb Kakoso baada ya kuishinda bao mbili kwa sifuri timu ya Sijonga FC.

MKUU wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu leo Aprili 27,2023 amehitimisha mashindano ya Muungano CUP yaliyokuwa yanalindima wilayani humo kwa kukabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi.

Timu ya Majalila FC imeibuka mshindi wa kwanza wa mashindano hayo, katika fainali iliyochezwa katika Uwanja wa michezo Majalila shule ya msingi kwa kuitandika Sijonga FC bao mbili kwa bila.

Akihutubia wakazi wa mji wa Majalila mara baada ya kumalizika kwa fainali kati ya Majalila FC dhidi ya Sijonga FC, DC Buswelu amewapongeza washiriki wote wa mashindano hayo, kwani ni njia moja wapo ya kudumisha mshikamano kama ilivyo asisiwa na waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere na Hayati Abeid Karume.

DC Buswelu amesema kutokana na jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika michezo, Serikali wilayani Tanganyika imekusudia katika bajeti yake ya Mwaka wa fedha huu kutenga fedha kwa ajili ya kujenga Uwanja wa kisasa wa mpira.

Kwa upande wake Kaimu mkuu kitengo cha michezo Halmashauri ya Tanganyika, Otuman Kasamya amesema katika mashindano hayo mshindi wa kwanza ambaye ni Majalila FC amepata zawadi ya shilingi elfu Themanini na kikombe, mshindi wa Pili shilingi elfu Hamsini, mshindi wa Tatu shilingi elfu 30 huku mshindi wa Insha akijipatia zawadi ya shilingi elfu Ishirini ambaye ni mwanafunzi kutoka Kakoso Sekondari na mwamuzi bora aliyejioatia shilingi elfu Ishirini.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment