Monday 8 May 2023

WILAYA YA TANGANYIKA: YAWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KWA AJILI YA KILIMO NA MIFUGO.





HAYO yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mheshimiwa Onesmo Buswelu alipoitembelea kampuni ya Meru Agro Wilayani Mbozi akiwa pamoja na kamati ya ulinzi ya Wilaya, Waheshimiwa Madiwani na Wakuu wa Idara.

Ziara hiyo ilifanyika Tarehe 05/05/2023 hadi Tarehe 7 ikiwa ni kuitembelea kampuni ya Meru Agro kuona namna inavyozalisha mbegu Mbalimbali, viuatilifu na vifaa vya shambani.

Mheshimiwa Buswelu alisema "Nawaomba Muje muwekeza Tanganyika, ardhi ipo ya kutosha, usalama upo na wataalam wa kufanya nao kazi wapo". Pia alisisitiza kufanya tafiti za udongo katika eneo la Wilaya hiyo ili kujua ni mbegu zipi zinafaa kutumika katika eneo hilo.

Kwa upande wake Christopher Shimwela, Meneja wa kampuni ya Meru Agro kanda ya Mbeya, alisema msimu uliopita walizalisha mbegu tani elfu tano na zote ziliisha. "Na Msimu huu tunategemea kuzalisha tani zaidi ya elfu sita"

Pia Mkurugenzi wa Meru Agro Ndugu Matanga Chacha alisema "Tupo tayari kuwekeza Tanganyika na tumeagiza mitambo ya thamani ya Shilingi Billioni 2 itakayotumika katika kilimo Wilayani Tanganyika" pia aliomba apewe ekari elfu tano kwa ajili ya uwekezaji huo.

Shabani Juma Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika alimuhakikishia muwekezaji huyo kutoa eneo la ekari elfu tano kama atafuata vigezo vilivyowekwa na Wilaya hiyo pamoja na kamati ya uwekezaji.

Pia msafara wa Mkuu wa Wilaya na Madiwani pamoja na wakuu wa Idara ulipata nafasi ya kutembelea Shamba la Mahindi lenye ekari elfu tatu lililopandwa mahindi aina ya Meru HB 515, Meru HB 513, Meru HB 405 na Meru HB 623 pamoja na mbegu za mahindi ya asili aina ya Situka M1.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Ahmed Mapengo alimtaka muwekezaji huyo kuwa na nia ya dhati kuwekeza katika eneo hilo. "kumekuwa na watu wengi wababaishaji na hawana nia ya kufanya uwekezaji, wanapewa maeneo na wanayatelekeza" Alisema

Wilaya ya Tanganyika imetenga eneo la Luhafwe lenye Hekta 46 elfu kwa ajili ya uwekezaji wa miundombinu ya Kilimo na Mifugo.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment