Monday 15 May 2023

DC TANGANYIKA AWATAKA WAZAZI KUTENGA MUDA WA KUZUNGUMZA NA WATOTO WAO.



MKUU wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu ametoa wito kwa wazazi kurudi enzi za nyuma kwa kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao mara kwa mara badala ya kuwawekea katuni kwenye runinga huku watoto wakiendelea kuharibika kimaadili.

DC Buswelu ametoa wito huo leo Mei 15,2023 katika maadhimisho ya Siku ya Familia duniani yaliyofanyika Kiwilaya katika viwanja vya Shule ya Msingi Ifukutwa, Halmashauri ya Tanganyika Mkoani Katavi.

Amesema yapo mambo yanafanywa na jamii yasiyompendeza Mungu kama mapenzi ya jinsia moja na vikiwemo vitendo vya ukatili, ukichunguza vinatokana na kukosekana kwa maadili  hivyo ipo haja ya wazazi na walezi kuwatengenezea misingi mizuri watoto wao kabla hawajaharibika.

Akilejea maneno ya Mungu katika Biblia, DC Buswelu amesema Mungu alipoona matendo maovu yamekithiri katika uso wa dunia, alichukia na kushusha gharika na sodoma na gomola ikateketea na watu wote, na ameitaka jamii kuachana na matendo maovu kabla Mungu hajachukia na kushusha gharika.

"Ili haya yatuepuke lazima turejee kwenye kuwekeza kwenye Utu, tuwekeze kwenye Ubinaadamu, tuwekeze kwenye Upendo, tuwekeze kwenye Umoja, tuyajenge maadili ya Taifa letu kuanzia ngazi ya Familia"

Mzee maarufu, Hassan Mapengo mkazi wa Tanganyika amesema zamani wazazi walikuwa na utamaduni wa kukutana na watoto wao ndiyo maana hapakuwa na matendo ya unyang'anyi, kuporomoka kwa maadili tofauti na sasa ambapo wazazi hawana muda wa kuzungumza na watoto zaidi wanarudi usiku.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment