Wednesday 11 July 2018

Waziri wa maliasili na utali afanya utalii Nkondwe



Posted On: July 10th, 2018
Halmashauri ya wilaya ya Mpanda imepongezwa kwa kutunza na kuhifadhi misitu ya Tongwe mashariki, Nkamba na misitu ya vijiji.
Pongezi hizo zimetolewa na waziri wa maliasili na utalii mhe. Dkt Hamis Kigwangala, Julai 09, 2018 alipofanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya wilaya ya Mpanda (Tanganyika). Baada ya kupokea taarifa iliyowasilishwa na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika mhe. Salehe mhando, taarifa hiyo ilisheheni  fursa za utalii zinazopatikana katika Halmashauri ya wilaya ya Mpanda na umahili mkubwa wa kuhifadhi misitu.
Fursa hizo ni pamoja na eneo la Karema linalopatikana katika mwambao wa ziwa Tanganyika ambapo Daktari wa kwanza mwafrika aliishi pale na kuzikwa Karema.
Hata hivyo, Dkt. Kigwangala alioneshwa eneo la uwekezaji lenye ukubwa wa hekta 46,000 ambapo kuna eneo lililotengwa kwa ajili ya  utalii ikolojia. Eneo hilo la utalii ikolojia lina maporomoko mazuri katika mlima wa Nkondwe, sokwe mtu, vipepeo vya rangi za kipekee na vivutio vingi vya kitalii.
Baada ya kufika katika maporomoko hayo, msafara ulielekea katika msitu wa Tongwe Mashariki ambao unamilikiwa na kulindwa na Halmashauri ya wilaya ya Mpanda. Baada ya kujionea kwa macho namna msitu ulivyofunga na kulindwa kwa umakini, msafara ulielekea katika msitu wa Tongwe Magharibi.
Msitu wa Tongwe Magharibi umezungukwa na vijiji 11 vya Halmashauri ya wilaya ya Mpanda. Halmashauri ya wilaya ya Mpanda imeomba kukabidhiwa msitu huo wa Tongwe Magharibi kwani ina uwezo wa kuulinda na kuuhifadhi. Msitu wa Tongwe Magharibi ni chanzo cha mito 16 inayotiririsha maji yake katika Halmashauri ya wilaya ya Mpanda na mjawapo wa mito hiyo ni pamoja na mto Katuma na Mnyamasi.
Halmashauri ya wilaya ya Mpanda kwa kushirikiana na wadau wa utunzaji wa mazingira hasa Taasisi ya Jane Goodall, Tuungane na FZS wamekuwa wakisaidia sana kutoa fedha za kufanya matumizi bora ya ardhi. Hadi sasa vijiji 23 kati ya 55 vimefanya matumizi bora ya ardhi.
Aidha, wananchi wameelimishwa vya kutosha juu ya utunzaji wa mazingira hasa misitu na vijiji 9 vinatarajia kuingia katika makubaliano ya kuuza hewa ya ukaa muda wowote kuanzia sasa.

No comments:

Post a Comment