Sunday 22 January 2023

MIGOGORO INACHELEWESHA MAENDELEO - DC BUSWELU.


Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu akihutubia Wananchi waliojitokeza viwanja vya Shule ya Msingi Mpanda Ndogo Kijiji cha Majalila Kata ya Tongwe wakati akizindua Wiki ya Sheria Wilayani humo.


MKUU wa wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi Onesmo Buswelu ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule ili hapo baadae Taifa liweze kupata Mahakimu na Majaji wa kutosha.

Ametoa wito huo wakati akizindua wiki ya sheria kiwilaya leo Januari 22,2023 alipokuwa akihutubia Wananchi waliojitokeza eneo la viwanja vya Shule ya Msingi Mpanda Ndogo Kijiji cha Majalila Kata ya Tongwe.

Pia DC Buswelu ametoa wito kwa Mahakimu na watoa huduma wote katika wiki ya sheria maeneo mbalimbali wilayani humo kutumia nafasi hiyo kuwaelimisha wananchi umuhimu wa elimu na kuwakumbusha kuwa mtoto kupata elimu ni takwa la kisheria.

Aidha, amehimiza Wananchi kutumia fursa hii ya wiki ya sheria kujitokeza kueleza changamoto zinazowakabili badala ya kukaa na migogoro bila suluhu hali ambayo inaweza kupelekea kujichukulia sheria mkononi.

"Migogoro inachelewesha maendeleo, nitoe wito kwa wananchi, Mkisikia matangazo haya jitokezeni njooni mpate elimu bure hamtalipia kwa sababu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anatoa mishahara, anatoa uwezeshaji ili (Mahakimu) waweze kuwafikia. NJOONI MPATE ELIMU HII BURE"


Katikati ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria wilaya ya Tanganyika ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu, Kulia ni Shaban Juma Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tanganyika na kushoto ni Glory Mwakihaba, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika.

Kwa upande wake Glory Mwakihaba, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi amesema moja ya changamoto walizobaini ni pamoja na wananchi walio wengi kutopenda njia ya usuluhishi  kwa kuamini kuwa kazi ya mahakama ni moja tu ya kufunga watu gerezani.

Amesema kupitia wiki ya sheria watapata nafasi ya kuwaelimisha wananchi kuwa usuluhishi ni njia bora na rahisi katika utatuzi wa migogoro inayotumika duniani na kuwaondoa hofu kuwa kesi huchelewa kukamilika na kuchukua muda mrefu ni kwa sababu ya kufuata sheria na taratibu za usuluhishi ili uamuzi unapotolewa pande zote zipate haki.

Hata hivyo amesema kuwa katika Wilaya hiyo kwa muda mfupi waliofanya kazi wamebaini kuwa vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, matukio ya ukatili wa kijinsia, mauaji zikiwemo mimba za utotoni ni matukio yanayo ongoza kujirudia mara kwa mara hivyo watajikita katika kutoa elimu zaidi kwa wananchi.


Glory Mwakihaba, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.


Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wameshukuru kwa kuogezewa huduma ya sheria karibu huku wakisisitiza changamoto walizonazo hasa vitendo vya ukatili.

"Tunashukuru kwa sisi wakazi wa hapa maana changamoto tulizonazo ni nyingi sana, ukiangalia vitendo vya kikatili vinavyotendeka ni vingi sana tulikuwa tunafikiria tutayapeleka wapi malalamiko yetu"- amesema Noriath Kakuta,mkazi wa kitongoji cha Majalila.

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu: wajibu wa Mahakama na wadau" ambapo uzinduzi huo Kitaifa umezinduliwa Jijini Dodoma na Mgeni Rasmi akiwa ni Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango.

Kauli hii imebeba ujumbe muhimu kuhusu wajibu wa mahakama na wadau katika kutumia njia ya usuluhishi kutatua migogoro kwa lengo la kukuza uchumi endelevu ambapo wiki hii ya Sheria ni wakati wa Mahakama na wadau  kuwaelimisha wananchi faida za kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi.




MWISHO.

No comments:

Post a Comment