Tuesday 24 January 2023

KAMATI YA SIASA (CCM) WILAYA YA TANGANYIKA YAWATAKA WATUMISHI KUSIMAMIA ILANI.



Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanganyika Yasin Kiberiti akieleza jambo baada ya kamati ya siasa kumaliza ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika kituo cha Afya Ipwaga.

KAMATI ya siasa ya Chama Cha  Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanganyika ikiongozwa na Mwenyekiti wake Yasin Kiberiti Jana Januari 23,2023 imeanza ziara ya siku tano ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo.

Wakiwa katika mradi wa ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika kituo cha Afya Ipwaga, Mwenyekiti Kiberiti amesema ameridhishwa na hatua ambayo miradi yote waliyotembelea imefikia huku akisisitiza usimamizi zaidi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.

Aidha, ametoa wito kwa viongozi ambao ni wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kusimamia Ilani ya CCM kwa kile alichodai dhamira ya chama hicho ni kuhakikisha wananchi wanafaidi matunda ya chama hicho.

"Serikali yetu iko makini na ni jukumu letu Chama Cha Mapinduzi kuisimamia Serikali na kuishauri"
Picha mbalimbali zikiwaonyesha wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Tanganyika na Wataalam.

Pia ameshauri halmashauri kusaidia fedha ili kuboresha ujenzi wa mradi wa Zahanati Kijiji cha Kapemba unaotekelezwa kwa fedha za mfuko wa jimbo ambao toka mwaka 2017 mradi uanze kujengwa hadi sasa mradi huo umekwama katika hatua za umaliziaji.

Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambaye pia ni Afisa mipango Deus Luziga amesema  Halmashauri iko tayari kuwaunga mkono wananchi katika miradi iliyoanzishwa kwa nguvu zao endapo watazingatia utaratibu wa kufikisha mradi hatua ya lenta.

Kamati hiyo jana imetembelea mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mganga Kijiji cha Kapemba wenye thamani ya Tsh. Milioni 50 sambamba na ujenzi wa mradi wa zahanati ya Kijiji hicho, ujenzi wa mradi wa maji vijiji vya Isenga, Ifumbura na Kapemba unaoghalimu zaidi ya Tsh. Bilioni 1.3, mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Isubangala.

Miradi mingine ni ujenzi wa Zahanati ya Kijiji Mganza iliyoibuliwa kwa michango ya Wananchi na mradi wa ujenzi wa jemgo la wagonjwa wa nje (OPD) katika kituo cha afya Ipwaga.



Picha ya kwana ni Mradi wa Nyumba ya Waganga iliyojengwa kwa ajili ya Watumishi watakaohudumia katika Zahanati inayojengwa Kijiji cha Kapemba (picha ya Pili) kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo.



Picha namba moja ni ujenzi wa mradi wa tenki la maji vijiji vya Isenga, Ifumbura na Kapemba unaoghalimu zaidi ya Tsh. Bilioni 1.3. Picha namba Mbili ni chanzo cha maji kitakachotumika katika tenki hilo.

Mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Kituo cha Afya Ipwaga.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment