Monday 30 January 2023

TANGANYIKA YAVUKA LENGO LA KITAIFA LA KUPANDA MITI MILIONI 1.5 KILA HALMASHAURI.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu kwenye Picha ya pamoja na Wakuu wa Idara mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Tangayika, Wanafunzi na baadhi ya Wananchi baada ya kumaliza zoezi la kupanda miche ya Miti 350 katika Makazi ya Watumishi Majalila.


HALMASHAURI ya wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi leo januari 30,2023 imeendelea na zoezi la upandaji miti ambapo mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amewaongoza Wakuu wa Idara mbalimbali na baadhi ya wananchi kupanda miti katika nyumba za Watumishi zilizopo eneo la Majalila.

Miti hiyo imepandwa pembezoni mwa Barabara ya Polisi kuelekea mtaa wa nyumba za Watumishi.

Mkuu wa wilaya Onesmo Buswelu amesema jumla ya miti 350 imependwa leo eneo hilo na kufanya jumla ya miti iliyopandwa katika halmashauri ya wilaya ya Tanganyika hadi sasa kufika Miloni 214,750 na kuifanya halmashauri hiyo kuvuka lengo la kitaifa linaloitaka kila halmashauri kupanda miti isiyopungua Milioni 1.5

"Nitoe wito kwa wasimamizi wetu wote, Viongozi wote kusimamia miti hii istawi vizuri. Tunatamani miti hii usife mti hata mmoja na isife lazima itunzwe na ilindwe"





Picha mbalimbali zikiwaonyesha wakuu wa Idara Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika katika zoezi la upandaji Miti katika Nyumba za Watumishi.

Aidha, amewaonya wenye mifugo kulisha kwenye miche iliyopandwa na mazao ya wakulima pamoja na Wananchi wanaong'oa na kuiba miche iliyopandwa kuacha tabia hiyo mara moja.

Nae Meneja TFS Wilaya ya Tanganyika Saimon Peter amesema zoezi hilo ni endelevu katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo licha ya kuwa wameshavuka lengo kwani miti bado ipo kwenye vitalu na watahakikisha inasambazwa kwenye Taasisi mbalimbali ili ipandwe.
Meneja TFS Wilaya ya Tanganyika Saimon Peter akielezea zoezi la upandaji Miti katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Katika hatua nyingine, DC Buswelu amemtembelea mkulima wa Mahindi, Karanga, Alizeti, Pamba na Tumbaku Bw. Abdalah Kakoso na kushuhudia uwekezaji mkubwa uliofanywa na mkulima huyo, hii ikiwa ni ukaguzi wa jitihada za Serikali baada ya kutoa mbolea ya ruzuku kama imefanyiwa kazi sawa na malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwakwamua wakulima.

DC Buswelu amempongeza mkulima huyo na kutoa wito kwa maafisa Kilimo kuendelea kutoa ushauri kwa wakulima ili Kilimo chao kiwe na tija.





Kwa upande wake Abdalah Kakoso ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha wakulima kupata mbolea ya ruzuku tofauti na mwanzo ilivyokuwa inauzwa kwa bei holela hali iliyowafanya washindwe kupanua kilimo chao.

"Nimshukuru sana Rais wetu Mama Samia amefanya kazi nzuri sana kwenye Kilimo kwani tulikuwa tunanunua mbolea shilingi 140,000 mfuko mmoja lakini ametoa ruzuku kwa hiyo sasahivi ni elfu sabini nafikiri kila mkulima anajitahidi kununua"

Pia ameishukuru Serikali ya Tanganyika kwa kuwa karibu na wakulima hasa kitendo cha Mkuu wa wilya kumtembelea kimpempa nguvu na kuahidi kufuata maelekezo na ushauri anaopewa.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment