Tuesday, 24 January 2023

DC JAMILA AHIMIZA UPANDAJI NA UTUNZAJI WA MITI HALMASHAURI YA WILAYA TANGANYIKA.


Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa upandaji Miti Wilaya ya Tanganyika lililofanyika Shule ya Sekondari Majalila akizindua zoezi hilo kwa kupanda mche wa Mti aina ya Mparachichi.

MKUU wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf leo Januari 24,2023 amewaongoza wakazi wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika shule ya sekondari Majalila ikiwa ni mwendelezo wa upandaji Miti milioni 2,014,000 katika Halmashauri hiyo.

DC Jamila amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais ikishirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imeendelea kuratibu utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji na utunzaji wa miti inayotekelezwa nchini kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Amesema "kila Halmashauri imewekewa malengo ya kupanda miti isiyopungua Milioni 1.5 kwa mwaka 2022/23 na kuhakikisha maeneo yote yaliyotengwa katika shughuli za uhifadhi yanahifadhiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoukabili ulimwengu kwa sasa".




Sambamba na hayo Jamila ameagiza kuchukuliwa hatua kwa yeyote atakayekamatwa akiharibu mazingira huku akionya siasa kutoingizwa kwenye suala zima la utunzaji wa mazingira.

"Yeyote anayeleta hitilafu, uharibifu wa mazingira asiangaliwe usoni, hata kama ni Kiongozi mwenzetu awajibishwe kwa mujibu wa sheria"

Kupitia hafla hiyo, DC Jamila ametoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika,Wakala wa Misitu (TFS) na Wakala wa Maji vijijini (RUWASA) kuainisha maeneo yote ya vyanzo vya maji kisha iwekwe mikakati ya kupanda miti kuzunguka vyanzo hivyo.

Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Afisa maliasili na utalii Wilaya ya Tanganyika, Bruno Nicolaus amesema jumla ya miche milioni 2.14 ya miche ya matunda, Kivuli na mbao ilioteshwa mwaka 2022 kwa ajili ya kupandwa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo.

Mkoa wa Katavi leo Januari 24,2023 umezindua zoezi la upandaji Miti litakalofanyika kila Halmashauri ambapo kilele chake kitahitimishwa Manispaa ya Mpanda tarehe 26,2023 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko.


No comments:

Post a Comment