Saturday 11 February 2023

CCM TANGANYIKA YAAHIDI USHIRIKIANO KUFIKIA MALENGO YA KUKUSANYA BILIONI 40.3

MWENYEKITI wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi Yasin Kiberiti amesema hana wasiwasi na halmashauri ya Tanganyika kufikia na hata kuzidi lengo la kukusanya na kutumia Tsh. Bilioni 40.3 endapo vyanzo vya mapato vitasimamiwa vizuri.

Ameyasema hayo katika kikao cha baraza maalumu la madiwani la kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya mwaka 2023/24, kikao kilichofanyika Jana Februari 10, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Mkurugenzi.

"Na sisi tutakutana na wenzetu Ofisi ya Mkuu wa wilaya kwa maana ya kusimamia bajeti kuhakikisha mapato yote tuliyojiwekea, mamilioni haya tuliyojiwekea yanakamilika lakini yanazidi hizo asilimia. Tukisimamia vizuri naamini hizo zitazidi"

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi Yasin Kiberiti.

Naye Katibu Tawala wilaya ya Tanganyika Geofrey Mwashitete amesema ili kufikia malengo hayo wataandaa mazingira mazuri kwa mamlaka za Serikali za mitaa ikiwemo kutoa ushirikiano.

"Kwa kweli inaonekana ni bajeti nzuri na kubwa kwa sababu kama mwaka huu mapato ya ndani imepangwa Bilioni 10 na milioni 12 ikilinganishwa na mwaka jana tulikuwa kwenye Bilioni tano na kidogo kwa hiyo tumepaa na tafsili yake ni kwamba mambo mengi yatatekelezwa"

Katibu Tawala wilaya ya Tanganyika Geofrey Mwashitete.

Akihitimisha kikao hicho Mwenyekiti wa halmashauri ya Tanganyika Hamad Mapengo amewashukuru madiwani kwa michango yao pamoja kuipitisha rasimu ya bajeti ya mwaka 2023/24 iliyowasilishwa na Afisa mipango wilaya ya Tanganyika Deus Luziga.

Aidha, amesema mapendekezo yote yaliyopendekezwa ikiwemo kuongeza vyanzo vya mapato vitazingatiwa kwa kuwa vitaiongezea halmashauri mapato jambo litakalowezesha kutekeleza miradi mbalimbali hadi ya ziada.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Tanganyika Hamad Mapengo.




Sehemu ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment