Thursday 2 February 2023

MWENYEKITI CCM WILAYA YA TANGANYIKA: WATENDAJI TIMIZENI WAJIBU WENU.


Pichani ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanganyika Ndg. Yasin Kiberiti iliyochukuliwa wakati wa ziara.

Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi imesema wajumbe wanapofanya ziara ya kukagua miradi ni kutaka kujiridhisha utendaji kazi wa Watumishi na usahihi wa matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama hicho wilaya ya Tanganyika Yasin Kiberiti katika kikao cha majumuisho baada ya ziara ya siku Tano katika Kata 14 iliyofanywa na kamati hiyo kumalizika.

Kiberiti amesema katika ziara hiyo wamebaini wapo baadhi ya watumishi hawakai kwenye vituo vyao vya kazi na wengine wapo lakini hawatekelezi wajibu wao wa kuwatumikia wananchi.

Aidha, kamati imebaini ubadhilifu wa wizi wa vifaa vya ujenzi ambapo katika baadhi ya miradi wamekuta ndoo nne za rangi zimeibwa.

"Wapo baadhi ya Watumishi walioko huko chini hawakai kwenye vituo vyao, hilo tumeshalibaini tunalo. Kuna baadhi ya Watumishi hawatekelezi wajibu wao maana yupo kama Mwananchi wa kawaida na kila kinachofanyika yeye hajui"

Amesema watu wa namna hiyo wanaweza kumsababishia Mkurugenzi Mtendaji  shida kwa kuwa usimamizi wao kwenye miradi ya Maendeleo ni hafifu.

Akiwasilisha mapendekezo ya kamati katika baadhi ya miradi waliyotembelea Katibu wa CCM wilaya ya Tanganyika Ndugu Adelaida Paskal Machenchewa amesema kamati imependekeza fedha itafutwe popote ili kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kapemba na iweze kutoa huduma zinazostahili kutolewa.

Pia kamati imependekeza kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo Mradi wa maji vijiji vya Isenga, Ifumbura na Kapemba unaoghalimu zaidi ya Tsh. Bilioni 1.3 ambapo mradi umefikia asilimia 60 na mradi unapaswa kukamilika Machi 30,2023 sambamba na miradi mingine.

Pamoja na hayo, kamati imeipongeza Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hssan kwa kutenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bweni la wanafunzi shule ya sekondari Kabungu wenye thamani ya zaidi ya Tsh. Milioni 69.

"Kamati ya siasa ya  chama cha Mapinduzi licha ya kupongeza, iliomba na kuagiza wanafunzi wote waliotakiwa kuripoti katika shule ya sekondari Kabungu waripoti"

MWISHO

No comments:

Post a Comment