Sunday 5 February 2023

UJUMBE WA CCM MKOA WA KATAVI KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 46.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi Comred Idd Kimanta,mgeni rasmi katika maadhimisho ya Miaka 46 ya CCM.

Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi Comrade Idd Kimanta amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho mkoani Katavi kuacha majungu badala yake watengeneze mahusiano mazuri na Watumishi kwa kuwa wao ndio watekelezaji wa Ilani.

Kimanta ametoa kauli hiyo leo akiwa Kijiji cha Mpembe kitongoji cha Kabatini halmashauri ya wilaya ya Tanganyika akihutubia Wananchi wa kitongoji hicho katika kelele cha maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa chama hicho.

Amesema kamati ya siasa mkoani humo haitasita kumchukulia hatua Kiongozi wa chama ambaye atabainika kuvuruga mahusiano baina ya Serikali na chama hali kadhalika kwa Mtumishi atakayebainika kuvuruga mahusiano baina ya chama na Serikali.

"Sisi wote ni Binadamu kukitokea kutoelewana basi kutoelewana huko kuzungumzwe kwa kuheshimiana, hatutarajii tufike mahali tukute Kiongozi wa chama au Kiongozi wa Serikali anamdharau mwenzake"

Amesema pamoja na kuisimamia Serikali lazima chama hicho kiilinde kwa kuiunga mkono huku akimtaka Mkuu wa mkoa huo kuwachukulia hatua Watumishi wote wazembe wanaokwamisha maendeleo ya Mkoa na ilani ya chama.

"Kwenye tenga samaki mmoja akioza toa yule aliyeoza halafu wale wengine waendelee wawe kitoweo. Mtumishi mmoja asiharibu sifa ya Watumishi wengine, toa yule wengine wazuri tunaendelea kuwa nao hakuna cha samaki mmoja akioza wote wameoza"

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi Comred Idd Kimanta akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko.

Aidha, ametoa wito kwa wana CCM kutambua wajibu wao na kufanya ziara kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua huku akiwasihii Watanzania kuendelea kuwa na imani na chama cha mapinduzi kwa kuwa ndicho chama pekee kinachoweza kutatua kero zao.

"Chama kinapokwenda ndani ya wananchi kinasikia nini wananchi wanataka. Chama lazima kila siku kisikie wananchi wanataka nini kwa sababu chama ndio kimbilio la wananchi"

Pamoja na yote, chama cha (CCM) Mkoa wa Katavi kimehitimisha maadhimisho hayo kwa kuwakabidhi kadi za uanachama wanachama wapya 2700.

Chama cha Mapinduzi (CCM) leo Februari 5,2023 kinaadhimisha Miaka 46 toka kuanzishwa kwake Februari 5, 1977.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi Comred Idd Kimanta akikabidhi kadi kwa mmoja wa wanachama wapya.





No comments:

Post a Comment