Sunday 5 February 2023

RC KATAVI ATAJA MAFANIKIO YA MKOA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 46 YA CCM.

MKUU wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema kwa kipindi cha Miaka miwili na nusu chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoa na taasisi zake umetumia zaidi ya Tsh. Bilioni 620 katika kutekeleza miradi mbalimbali.

Mhe. Mrindoko amesema katika sekta ya elimu mkoa umepata vyumba vya madarasa 119 katika shule za sekondari na kuwezesha wanafunzi 14,854 waliofaulu kidato cha kwanza kuweza kupata Sehemu ya kusomea.

Amesema sekta ya afya mkoa wa Katavi umepata Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambayo imeanza kutoa huduma, Hospitali 5 za wilaya, vituo vya Afya zaidi ya 14 na Zahanati zaidi ya 20 ambapo miradi hiyo yote imetekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani, Serikali kuu na zingine kutoka kwa wafadhili na wadau mbalimbali.

Mhe. Mrindoko ametaja mafanikio mengine ya chama cha mapinduzi katika sekta ya maji kuwa mkoa wa Katavi umefikia asilimia 70.7 ya upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 60 mjini huku Mpanda mjini ikitarajia kufikisha asilimia 100 ya upatikanaji wa maji kupitia mradi wa "miji 28" unaotarajia kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha.

Kadhalika RC Mrindoko amesema katika sekta ya miundombinu yapo mafanikio makubwa ikiwemo mkoa kuunganishwa na mikoa mbalimbali kwa kiwango cha lami na kiasi cha Tsh. Bilioni 4 kinatarajiwa kutumika kukarabati barabara za miji na vijijini kupitia TARURA ikiwemo ujenzi wa madaraja makubwa likiwemo daraja la Mto Msadya na daraja la Ifinsi.

"Mheshimiwa mwenyekiti kama ulivyotuagiza barabara hii ya inayoingia eneo la Kabatini ni barabara ambayo ina hali mbaya, nikuhakikishie barabara hii imetengewa Milioni 200 katika mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai 2023 barabara hii itaweza kufanyiwa matengenezo"


Mafanikio mengine ni kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo migogoro 74 ambayo ipo kwenye timu ya Mawaziri nane imeweza kuwasilishwa na migogoro hiyo ipo katika hatua za mwisho za utatuzi.

Aidha, aametoa wito kwa wananchi kutunza Misitu.


Baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kuadhimisha Miaka 46 ya CCM katika viwanja vya Shule ya Msingi Kabatini leo Februari 5,2023.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment