Thursday 9 March 2023

SERIKALI KATAVI KUENDELEA KUIMARISHA UWEZESHAJI WANAWAKE.

MKUU wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema serikali itaendelea kutoa uwezeshaji kwa wanawake kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wanawake kushiriki katika biashara na uzalishaji.

Akihutubia katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani Machi 8, 2023 yaliyoadhimishwa kimkoa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mpanda Ndogo wilayani Tanganyika, Mrindoko amesema licha ya mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa wanawake, serikali itaendelea kuimarisha maeneo ya biashara yatayowavutia wanawake.

Aidha amewasisitiza wanawake kujielimisha katika kutambua haki zao ikiwemo haki ya kumiliki mali hasa ardhi, haki ya kupata elimu na usawa katika kufanya kazi.





Awali akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi Afisa maendeleo Msaidizi wa mkoa wa Katavi, Kennedy Wilson amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita halmashauri za mkoa huo zimetoa mikopo kwa vikundi vya wanawake yenye jumla ya shilingi bilioni 1.5 

Aidha amesema katika mwaka wa fedha unaoendelea wa 2022/23 Halmashauri za mkoa wa Katavi tayari zimeshatoa mikopo yenye jumla ya shilingi 339.3 kwa vikundi 49 vya wanawake. 

Wilson amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao wa 2023/24 halmashauri za mkoa wa Katavi zinatarajia kutoa mikopo inayofikia shilingi milioni 547.9 kwa vikundi mbalimbali vya wanawake mkoani humo.

Afisa maendeleo Msaidizi wa mkoa wa Katavi, Kennedy Wilson.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mrindoko amesema Serikali mkoani Katavi haitasita kumchukulia hatua mwajiri yeyote atakayebainika kutoa ajira kwa kumbagua Mwanamke kutokana na jinsia yake.

''Kama kutakuwa na mwajiri yeyote ambaye atatoa haki kwa kubagua Mwanamke sio kwa karne tuliyonayo sasahivi, hatutamvumilia mwajiri yeyote ambaye atakosesha haki ya mtumishi Mwanamke kwa kumbagua kwa sababu yeye ni Mwanamke'' Alisema RC Mrindoko.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka huu yamepambwa na kaulimbiu inayosema  "UBUNIFU WA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA: CHACHU KATIKA KULETA USAWA WA KIJINSIA"

MWISHO.

No comments:

Post a Comment