Tuesday 28 March 2023

TANGANYIKA: VIONGOZI WA KATA NA VIJIJI WAPEWA SEMINA YA USIMAMIZI WA MIRADI YA HEWA UKAA.

Baadhi ya Watendaji wakifatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo katika utekelezaji na usimamizi wa miradi ya Hewa Ukaa yanayofanyika katika Ukumbi wa Mkurugenzi jengo la Halmashauri Machi 27,2023


VIONGOZI wa kata na vijiji vinavyonufaika na mradi wa hewa ukaa katika Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi leo wameanza mafunzo ya siku tatu yatakayohusisha mada mbalimbali ikiwemo dhana ya utawala bora na utunzaji wa nyaraka.

Akizungumzia yatakayojadiliwa katika mafunzo hayo Mratibu wa miradi ya hewa ukaa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Alfonce Mwakyusa amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa kata na vijiji pamoja na Wenyeviti wa vijiji ili kuimarisha usimamizi utakaozingatia utawala bora, namna ya kuibua miradi hiyo na matumizi sahihi ya fedha zitokanazo na mauzo ya hewa ukaa.

Ameongeza kuwa, fedha zinazotokelewa ni nyingi ambapo katika awamu hii ya Sita na Saba vijiji nane vinavyo nufaika na mradi wa hewa ukaa vimeingiziwa Tsh. Bilioni 4.27 hivyo kutakuwa na mada kuhusu uhandisi ujenzi na mada kuhusu masuala ya rushwa.

Bw. Alfonce Mwakyusa Mratibu wa miradi ya hewa ukaa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Akifungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Ukumbi wa Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewataka washiriki kuwa kutilia maanani mafunzo hayo kwani serikali haitataka kusikia Kijiji chochote kikienda kinyume au kuharibu mradi ikwemo udanganyifu katika kupata wazabuni.

"Yaani Vijiji vyoye 55 vifeli kuna Wilaya hapo? Wewe kwenye eneo lako unapotengeneza mikakati ya kufelisha maana yake unataka nchi yote ifeli. Unapotengeneza mikakati ya kuiba hata senti moja maana yake unataka nchi yote ifeli halafu mwisho wa siku tukimbile wapi? Mimi nawasihii, msifanye hivyo" 

Kataika hatua nyingine, DC Buswelu ameagiza kufikia Aprili mosi mwaka huu Vijiji vyote vunavyo nufaika na mradi viwe vimeingiziwa fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi.

Mhe. Onesmo Buswelu,Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika na mgeni rasmi katika mafunzo hayo akifafanua jambo.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wamesema wanaamini kupitia mada zinazowasilishwa wataenda kusimamia ipasavyo fedha na utunzaji sahihi wa nyaraka, usimamizi mzuri wa miradi kwani awali walikuwa hawana weledi na masuala hayo.



MWISHO.

No comments:

Post a Comment