Thursday 6 April 2023

TANGANYIKA: KISHINDO CHA SERIKALI YA AWAMU YA SITA NDANI YA MIAKA MIWILI YA UONGOZI WA RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN.


Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Tanganyika kwa kipindi cha miaka Miwili ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

ZAIDI ya shilingi Bilioni 131 zimekusanywa, kupokelewa na kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-25 katika Wilaya hiyo kwa kipindi cha miaka miwili( Machi 2021- 2023 ) cha serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ameyasema hayo katika kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Tanganyika kilichoketi Jana Aprili 5, 2023 katika ukumbi wa Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani humo.

DC Buswelu amesema fedha hizo shilingi 131,791,925,200.5 zimefanikisha kuifungua Tanganyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo Afya,  barabara, kilimo, elimu, maji, mawasiliano na uchukuzi, umeme vijijini, uwekezaji sanjari na sekta mbalimbali.

Katika sekta ya Afya ndani ya miaka miwili, wilaya hiyo ilipokea zaidi ya bilioni 4 ambazo zimetumika katika ujenzi wa miundombinu ya Afya kama ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi na ujenzi wa wodi tatu katika hospitali ya wilaya ya Tanganyika ikiwemo ujenzi wa vituo vya Afya, Zahanati na vyumba za watumishi.

Amesema, katika sekta ya barabara Wilaya ya Tanganyika sasa imeunganishwa na mtandao wa barabara hali inayochochea uwekezaji ikiwemo wananchi kujiingizia kipato kupitia usafiri na usafirishaji.

"Ujenzi wa barabara ya Vikonge - Luhafye yenye urefu wa KM 25 inayojengwa kwa fedha za kitanzania zaidi ya bilioni 35 mkandarasi yupo eneo la mradi na ujenzi unaendelea, barabara ya Kagwira - Ikola - Karema yenye urefu wa KM 120 ipo hatua ya awali ya upembuzi ambayo imefikia asilimia 95 na kiasi cha shilingi bilioni 1.073 kimetolewa" Alisema Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanganyika Yasin Kiberiti akifuatilia taarifa ya utekelezaji wa Ilani ikisomwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika




Baadhi ya Wajumbe wakifuatilia hotu ikisomwa kuhusu hatua ambayo Wilaya ya Tanganyika imepiga ndani ya kipindi cha miaka Miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan

Barabara nyingine zinazotengenezwa chini ya TANROAD ni ya Kibo - Mwese - Lugonesi, Kagwira - Karema na Mpanda - Uvinza huku Wakala wa mjini na vijijini TARURA akiongezewa bajeti kutoka 641,150,000 mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia 4,157,455,928.18 kwa mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 259.

Aidha, amesema sekta ya elimu imeimarika mara dufu baada ya kujengwa miundombinu ya kutosha  ambapo kupitia fedha za UVIKO-19 jumla ya vyumba vya madarasa 196 vimejengwa ( shule ya msingi  vyumba 127 na shule za Sekondari vyumba 69) na kupitia fedha za mapato ya ndani na hewa ukaa jumla ya vyumba 94 vimejengwa ikiwemo kujenga shule mpya ya Majalila, mabweni n.k

Pia chuo cha ufundi stadi (VETA) ujenzi wake unatarajia kuanza mwezi huu eneo la Kijiji cha Majalila.

Maeneo mengine aliyoyata wilaya hiyo kupiga hatua ni sekta ya maji ambapo shilingi 6,481,086,307.46 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji ambapo miradi 15 itakayonufaisha vijiji 22 inajengwa na baadhi imeanza kutoa huduma.

Hata hivyo, amesema sekta ya maliasili na utalii imezidi kuimarika ambapo kutokana na utunzaji na usimamizi mzuri wa maliasili na misitu, jumla ya vijiji 8 vya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika vimenufaika na mradi wa hewa ukaa ambapo shilingi bilioni 6.57 zimepatikana ndani ya miaka miwili.

Fedha hizo zimetumika kujenga madarasa, zahanati, kuajiri walimu wa mikataba, kutoa vyakula kwa wanafunzi shuleni, kuajiri Askari walinzi wa misitu na kukopesha vikundi vya wajasiriamali vijijini kupitia COCOBA.

Wilaya ya Tanganyika ilianzishwa mwaka 2016 ikijulikana wilaya ya Mpanda Vijijini ambapo jina la Tanganyika lilitokana na Ziwa Tanganyika lililopo kwenye mpaka wa mashariki ya eneo hili.

Katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, idadi ya wakazi wa wilaya ni 371836.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment