Thursday, 16 February 2023

RC KATAVI AAGIZA KUCHUKULIWA HATUA KALI WAZAZI AMBAO HAWAJAWAPELEKA WATOTO KUANZA MASOMO.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mridoko akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mwese.

MKUU wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Hoza Mridoko ameagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa wazazi ambao bado hawajawapeleka watoto kuripoti kidato cha kwanza.

Mkuu wa Mkoa Mrindoko ametoa agizo hilo katika ziara yake 10 Februari 2023 katika Shule ya Sekondari ya Mwese alipotembelea shuleni hapo kwa lengo la kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la Utawala lililojengwa kwa fedha zitokanazo na mradi wa Hewa ukaa.

“Nimeambiwa hapa Wanafunzi walioripoti ni 149 bado wanafunzi 15 hawajaripoti,muda uliotolewa na Serikali umekwisha pita,Nimtake Mhe. DC wa Wilaya hii ya Tanganyika hawa watoto watafutwe na wazazi wao wachukuliwe hatua,tunahitaji kujenga kizazi chenye maarifa na manufaa katika Taifa hili”,alisema Mkuu wa Mkoa Mrindoko.




Aidha Mhe.Mrindoko ametoa rai kwa  Wanafunzi Shuleni hapo kuunga mkono jitihada za Serikali  na kumtendea haki Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kusoma kwa bidii  kwa kuwa Serikali imetimiza kikamilifu wajibu wake wa kujenga mazingira wezeshi kwa Wanafunzi na Walimu  Nchini.

Amewataka Wanafunzi hao kutunza miundombinu ya Majengo pamoja na samani kusudi miundombinu hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu zaidi.

Katika hatua nyingne Mkuu wa Mkoa Mrindoko ameupongeza uongozi wa Shule ya Sekondari ya Mweze,Kamati za Ujenzi pamoja na Uongozi wa Kata ya Mwese kwa kusimamia ubora  na viwango katika ujenzi wa Jengo la Utawala Shuleni hapo.

Awali katika Taarifa yake Mkuu wa Shue ya Sekondari ya Mwese ameeleza kuwa mradi wa ujenzi huo ulianza utekelezaji wake Desemba 2021 ambapo hadi kukamilika kwake mradi  utagharimu kiasi cha shilingi Milioni Mia Moja arobaini ambapo hadi sasa Shilingi  Milioni mia moja thelathini na nane na laki nane  zimekwisha tumika  huku ujenzi ukiwa katika hatua za mwisho kabisa  za umaliziaji.

Katika hatua nyingine Wananchi wa Kijiji cha Kapanga Wilayani Tanganyika Mkoani Katavi wameeleza kushangazwa na kufurahishwa na utitiri wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya muda mfupi inayotekelezwa Kijijini hapo.

Wananchi wameeleza hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Hoza Mrindoko alipotembelea Kijiji hicho kwa lengo la kukagua mradi wa maji pamoja na Ujenzi wa Zahanati inayojengwa kupitia Fedha za Mradi wa Hewa Ukaa. Wananchi hao wameipongeza Serkkali ya awamu ya Sita chini ya Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo miradi mbalimbali ya maendeleo imekuwa ikitekelezwa Kjijijini hapo. Pamoja na Pongezi Wananchi hao walimueleza Mkuu wa Mkoa wa Katavi kuwa kwa sasa changamoto kubwa kijijini hapo ni upatikanaji wa Mtandao wa uhakika ambapo kwa muda mrefu Mawasiliano ya simu yamekua changamoto.
“Tunampongeza sana Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mingi ambayo inaendelea,changamoto yangu kubwa kwa sasa ni upatikanaji wa Mtandao na tumekuwa tukipata shida sana na hasa walimu ambao wamepatiwa vishkwambi wamekuwa wakipata changamoto ya mtandao,unawakuta wamerundikana sehemu moja wakitafuta mtandao. Hii ni shida ikipatiwa ufumbuzi mambo mengine yatakwenda” Alisema Zefania Sleni Mkazi wa Kijiji cha Kapanga.

Kufuatia changamoto hiyo Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko aliwatoa hofu Wananchi wa Kijiji hicho ambapo amewaeleza kuwa atalifikisha suala hilo kwa Waziri Mwenye dhamana ya Mawasiliano pamoja na kufanya ufuatiliaji wa karibu kusudi kupata ufumbuzi wa changamoto hiyo. Amewaeleza Wananchi wa Kapanga kuwa maendeleo yanayofanyika kijijini hapo ni jitihada za Serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan na kwamba hizo ni rasharasha tu mambo mazuri zaidi yanakuja.
Aidha amewataka Wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ushirikiano wa uhakika ikiwa ni pamoja na kulinda miundombinu ya Maji ili Wananchi waweze kunufaika zaidi na miradi hiyo.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment