Katibu Tawala Wilaya ya Tanganyika Geofrey Mwashitete.
WATENDAJI na watumishi wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wametakiwa kutimiza wajibu na kuzingatia maadili ya kazi kipindi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Tanganyika Geofrey Mwashitete katika kikao kazi cha kutoa mafunzo kwa watumishi, kilichoongozwa na Katibu huyo kilichofanyika eneo la shule ya Msingi Bulamata Kata ya Bulamata Tarafa ya Kabungu hapo jana Februari 16, 2023.
Mwashitete amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwapitisha watumishi kwenye kanuni, taratibu na sheria mbalimbali za utumishi wa umma ili waweze kutimiza wajibu wao.
"Tumepokea maagizo kutoka kwa waziri mkuu pamoja na Mh. Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza siku nyingi kwamba tunatakiwa siku 2 tuwepo ofisini lakini siku 3 twende tukasimamie miradi mbalimbali pamoja na kutembelea wadau pamoja na wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali"amesema
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwakumbusha watumishi wa umma kwamba muda mwingi wautumie kuwahudumia wananchi pamoja na wadau mbalimbali na viongozi wanaohusika kuhudumia wananchi kama maafisa ugani na afisa mifugo wafike kwa wananchi badala ya kusubiri kufuatwa maofisini.
Kwa upande wake Kaimu afisa utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Andrew Chiduo amesema kuwa lengo la kuwafuata watendaji na watumishi katika Tarafa hiyo ni kuwakumbusha haki na wajibu wao katika majukumu yao huku wakitarajia ufanisi zaidi katika kazi.
Kaimu afisa utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Andrew Chiduo.
Nao baadhi ya watumishi mara baada ya kupata mafunzo hayo wameahidi kuleta mabadiliko chanya katika majukumu yao kama watumishi wa umma.
"Tumekumbushwa mambo mengi ambayo mengine tuliyasahau, tumekumbushwa kudai haki zetu za msingi baada afisa utumishi kutukumbusha haki na wajibu ambao inatakiwa tupate na tufanye ili tupate haki zetu" amesema Justin Erasto,Afisa Mtendaji Kata ya Bulamata.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment