MKUU wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko Jana Machi 01, 2023 amezindua kampeni ya 'SHINDA MALARIA' inayotekelezwa katika Halmashauri mbili za Tanganyika na Nsimbo yenye lengo la kupunguza maambukizi, vifo na madhara ya kuugua Malaria hasa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na mama wajawazito.
Mradi wa 'SHINDA MALARIA' unatekelezwa na Taasisi ya afya ya Ifakara kwa ufadhili wa USAID|PMI.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, Mkurugenzi mkuu wa mradi wa 'SHINDA MALARIA' kutoka taasisi ya afya ya Ifakara Dkt. Dunstan Bishanga, amesema Mkoa wa Katavi ni kati ya mikoa Saba ambayo Wizara ya Afya imeitambua kama mikoa yenye maambukizi ya hali ya juu ya Malaria.
Amesema katika utafiti wa mwaka 2022 kwenye ngazi ya jamii ya ukubwa wa tatizo la Malaria ilikadiriwa watu 8 kati ya 100 mkoani Katavi wana vimelea vya Malaria.
Amesema katika kuhakikisha mapambano dhidi ya Malaria yanafanyika afua mbalimbali zinafanyika katika vituo vya Afya na ngazi ya jamii kwa kutoa huduma ya mkoba katika maeneo ambayo ni ngumu kufikika kwa kushirikiana na timu za uendeshaji na usimamizi wa afya za Mkoa na Halmashauri husika.
Dkt. Bishanga amesema katika kipindi cha miezi 7 mradi umetoa mafunzo kwa watoa huduma 36 watakaoweza kutoa huduma za Malaria ngazi ya jamii na watoa huduma waelimishaji 58 ikiwemo kuwapatia vitendea kazi.
"Umuhimu wa huduma hizi umejidhihirisha kwamba kati ya watu waliohudhuria hapa leo wameshapimwa mpaka sasa huduma zinaendelea watu takribani 100 na kati ya hao watu 3 kati ya watu 10 wamekutwa na vimelea vya Malaria, watu 3 kati ya 10 ni wengi sana katika takwimu za kawaida"
Mkurugenzi mkuu wa mradi wa 'SHINDA MALARIA' kutoka taasisi ya afya ya Ifakara Dkt. Dunstan Bishanga.
Nae mwakilishi wa USAID|PMI Lulu Msangi amesema toka mwaka 2020 PMI kwa kushirikiana na Serikali imesaidia uimarishaji wa ubora wa vituo vya Afya katika kutoa huduma bora za afya ambapo juhudi hizo zimepunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini kutoka asilimia 18 mwaka 2015 mpaka asilimia 8 mwaka 2020.
Aidha, ili kuendelea kupunguza ugonjwa wa Malaria mkoani Katavi PMI imetoa msaada wa vitendelea kazi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambavyo ni Baiskeli 21, Mikoba ya kuwekea vifaa 21, vipima joto 21, mizani ya kupimia uzito ya mgonjwa 21, masanduku 21 yaliyo na vifaa vya afya zikiwemo simu za mkononi 36 kwa ajili ya watendaji wa afya ngazi ya jamii na simu 26 za ziada vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 47.5
Lulu Msangi, mwakilishi wa USAID|PMI.
Kwa upande wake mgeni rasmi amepongeza na kushukuru wadau wote walioshiriki kuleta mradi huo katika Mkoa wa Katavi kwa kuwa ugonjwa wa Malaria ni kati ya tatizo linaloikabili nchi na katika kulinda heshima ya mradi huo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria ametoa wito kwa watoa huduma kuwa waadilifu katika kuwahudumia wananchi na atakaye bainika kwenda kinyume ikiwemo kutumia vibaya vifaa vilivyokabidhiwa atachukuliwa hatua za kisheria.
Pia amewataka wananchi kuacha imani potofu hasa kwa magonjwa ya mripuko ikiwemo Surua na kipindupindu badala yake wafike kwenye vituo vya Afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu ikiwemo chanjo mbalimbali za magonjwa ikiwemo chanjo ya Malaria, Surua na maradhi mengine.
Mrindoko amewaomba wafadhili wa mradi wa 'SHINDA MALARIA' kupanua wigo ili huduma hiyo itolewe katika Halmashauri zote tano za Mkoa huo.
Mradi huo unaofadhiliwa na USAID|PMI na kutekelezwa na Taasisi ya afya ya Ifakara ulianza kutekelezwa agosti 2022 na unatekelezwa kwa ufanisi katika Mkoa wa Katavi pekee Tanzania nzima kwa muda wa miaka mitano katika Halmashauri hizo mbili.
PICHA mbalimbali zikionyesha vifaa vilivyokabidhiwa na Mgeni rasmi.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment