WATU 09 wamefariki dunia na wengine 30 kujeruhiwa kutokana na ajali mbaya iliyotokea mlima mkali wa Nkondwe, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi baada ya basi aina ya Tata lenye namba za usajili T506 DHH kampuni ya Komba's kupinduka na kudondokea korongoni.
Taarifa ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Dkt. Alex Mrema imesema vifo hivyo tisa vimetokea papo hapo ambapo kati ya waliofariki wanaume ni 5 kati yao watu wazima ni 2 na watoto 3 na huku wanawake wanne wakipoteza maisha katika ajali hiyo akiwemo mjamzito.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Dkt. Alex Mrema akitoa taarifa ya Ajali kwa Mkuu wa Mkoa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi Ali Makame amesema ajali hiyo imetokea Machi 6, 2023 alasiri majira ya saa Tisa dakika 45 baada ya kufika katika mlima huo gari liliserereka na kudondokea kwenye korongo kubwa lenye kina cha mita zisizopungua 75.
Amesema hadi sasa chanzo cha ajali hakijajulikana na Jeshi la Polisi mkoani humo wanaendelea na uchunguzi huku zoezi la kuitambua miili likiendela kwa ajili ya taratibu zingine.
Picha mbalimbali za muonekano wa ajali ilivyo.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akiwa hospitali ya wilaya ya Tanganyika kuwajulia hali majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu, amesema kama Serikali imeguswa kwa ajali hiyo huku akitoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waliopoteza maisha kwani Taifa limepoteza nguvu kazi.
Aidha,amewapongeza viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika, wataalamu wa afya na Wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza haraka kusaidia kuwaokoa wale waliopata ajali.
"Kuna baadhi walikuja wakiwa na hali si nzuri lakini mara baada ya kupata huduma za afya hapa hospitali ya wilaya ya Tanganyika tayari hali zao zimeendelea kuimarika, tuendelee kuwaombea waliopata majeraha waweze kupona haraka"
Mhe. Mwanamvua Mrindoko, Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Moja ya majeruhi katika ajali hiyo Philbert Focus, mkazi wa Mpanda amesema wakati wamefika katika mlima huo ghafla kwenye kona gari lilienda kwa kasi kubwa kama limekatika breki ndipo lilipomshinda dereva na kuoitiliza kwenye korongo.
"Niliona kama giza baadae nikawa nimefumbua macho nikajikuta naumia nipo ndani gari limelala juu chini nikajikwamua kutoka japo kulikwa na kanafasi kadogo. Maumivu niliyopata ni ya mkono na michubuko kichwani na mguuni"
Philbert Focus, Majeruhi
Naye Hamadi Kambi shuhuda wa ajali hiyo amesema katika harakati za kushirikiana na Jeshi la Polisi kuokoa majeruhi, anasema ajali ilikuwa mbaya sana na katika kuokoa watu wanne wamefia mikononi mwake.
"Kuna mtoto mama yake kanifia mikononi, yule mtoto kanisikitisha sana"
Akiongea kwa niaba ya Wananchi, Mwenyekiti wa mtaa wa Luhafwe Raphael Lutonja amesema eneo hilo ni baya sana na mara kadhaa kumekuwa kukitokea ajali na kusababisha vifo huku akidai ajali iliyotokea leo ni mbaya zaidi kuliko ajali ambazo zimewahi kutokea eneo hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amewashukuru wanacnhi kwa kusaidiana na Serikali katika zoezi la uokoaji ikiwemo kujitolea vyombo vya usafiri kwa ajili ya kuwakimbiza majeruhi Hospitali.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment