Saturday 4 March 2023

WANANCHI WA MISHAMO WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUANZA UTEKELEZAJI MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI.


WANANCHI wilayani Tanganyika mkoa wa Katavi wameipongeza Serikali kwa hatua ya kuanza utekelezaji wa upimaji wa matumizi bora ya Ardhi kwani itasaidia kuleta amani na utulivu ikiwemo kuondoa migogoro hasa ya wakulima na wafugaji.

Pongezi hizo wamezitoa wakati timu ya wataalamu wa Ardhi mkoa wa Katavi wakiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ilipofika na kuzungumza na Wananchi wa kata ya Mishamo halamshauri ya wilaya ya Tanganyika juu ya mpango wa Serikali kutekeleza mpango huo.

"Nimefarijika na wenzangu na ujio wenu kuja kutuwekea huu utaratibu, bila shaka itaepusha mambo mengine ambayo yalikwa yanatukosesha amani na utulivu kwa kuwa mtakuja kutenga sehemu ya kilimo, sehemu za ufugaji watu wote tutaishi kwa amani na utulivu" Amesema Ndayegamiye Seth, mkazi wa Mishamo.
Ndayegamiye Seth, mkazi wa Mishamo.

Kwa upande wake Ibrahim Butta, Afisa mipango miji Mkoa wa Katavi amesema mpango wa matumizi bora ya Ardhi una manufaa kwa wananchi kwa kuwa Serikali hupeleka miradi sehemu nyenye mpangilio mzuri wa Ardhi kwa kuwa pia ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wanaishi katika mpangilio unaoeleweka.

Amesema mpango huo unasimamiwa na Wananchi wenyewe wakiwaongoza wataalamu kwa kuwa wao ndio wenye kuijua mipaka na kupendekeza matumizi ya Ardhi katika eneo lao na amewaomba wananchi kutoa ushirikiano pale wataalamu watakapopita kutoa elimu na kupata taarifa mbalimbali.
Afisa mipango miji Mkoa wa Katavi, Ibrahim Butta.

Nae Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwa suala la mipango bora ya Ardhi ndio ufunguo wa maendeleo Duniani kote kwani bila mpango huo migogoro itaendelea kuwepo na kusababisha kukwamisha maendeleo.

Ametoa wito kuwa makundi yote yashirikishwe katika zoezi zima la upangaji huku akiwaonya wote watakaobainika kuhujumu mpango huo.
Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu.

Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Nehemia James amesema kutokana na umuhimu wa zoezi hilo tayari Serikali ya mkoa imepata baraka kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na utekelezaji wake utafanyika eneo la makazi ya wakimbizi ya Mishamo na Katumba.






MWISHO.

No comments:

Post a Comment