Baadhi ya Viongozi waliohudhuria kikao cha DC na Wanahabari.
Wednesday, 16 August 2023
WILAYA YA TANGANYIKA IKO TAYARI KUUPOKEA MWENGE WA UHURU AGOSTI 24,2023.
Friday, 26 May 2023
DC BUSWELU AHIMIZA UKWELI KWENYE MAENDELEO AMBAYO SERIKALI INAYAFANYA
Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Tanganyika, ACP Kiberiti
DC Buswelu ametoa wito huo baada ya kutembelea na kukagua hatua ya ujenzi wa kituo cha Polisi Tanganyika, ambapo amsema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya Askari Polisi wilayani humo ikiwemo kuwajengea nyumba Watumishi wa Jeshi hilo.
Hayo yamejiri baada ya kauli ya Katibu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Salumu Mwalimu akiwa ziarani wilayani humo kutoa kauli ambayo siyo ya kweli kuwa OCD hana nyumba ya kuishi wakati viongozi wengine wamejengewa nyumba na Serikali.
"kuna nyumba kubwa imeshakamilika three in one. Polisi hawajasahaulika na kazi inaendelea vizuri wapo ambao tayari wameshahamia kwenye nyumba zile, nyumba zina maji na umeme"
Nyumba ya watumishi wa Jeshi la Polisi (Three in One)
Aidha, DC Buswelu amesema licha ya kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo, Serikali inajenga kituo cha kisasa cha Polisi kitakacho ghalimu shilingi milioni 500 ambapo ujenzi wake umefikia hatua ya kumwaga jamvi.
Kwa upande wake Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Tanganyika, ACP Kiberiti amesema kwa kiasi kikubwa uwepo wa nyumba hizo umesaidia wananchi kupata huduma ya kiusalama haraka.
ACP Kiberiti ameongeza kuwa, ujenzi wa kituo cha Polisi ulisimama kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha kutokana na jeografia ya wilaya hiyo hivyo ujenzi utaendelea hivi karibuni.
MWISHO.
Monday, 15 May 2023
DC TANGANYIKA AWATAKA WAZAZI KUTENGA MUDA WA KUZUNGUMZA NA WATOTO WAO.
DC Buswelu ametoa wito huo leo Mei 15,2023 katika maadhimisho ya Siku ya Familia duniani yaliyofanyika Kiwilaya katika viwanja vya Shule ya Msingi Ifukutwa, Halmashauri ya Tanganyika Mkoani Katavi.
Amesema yapo mambo yanafanywa na jamii yasiyompendeza Mungu kama mapenzi ya jinsia moja na vikiwemo vitendo vya ukatili, ukichunguza vinatokana na kukosekana kwa maadili hivyo ipo haja ya wazazi na walezi kuwatengenezea misingi mizuri watoto wao kabla hawajaharibika.
Akilejea maneno ya Mungu katika Biblia, DC Buswelu amesema Mungu alipoona matendo maovu yamekithiri katika uso wa dunia, alichukia na kushusha gharika na sodoma na gomola ikateketea na watu wote, na ameitaka jamii kuachana na matendo maovu kabla Mungu hajachukia na kushusha gharika.
"Ili haya yatuepuke lazima turejee kwenye kuwekeza kwenye Utu, tuwekeze kwenye Ubinaadamu, tuwekeze kwenye Upendo, tuwekeze kwenye Umoja, tuyajenge maadili ya Taifa letu kuanzia ngazi ya Familia"
Mzee maarufu, Hassan Mapengo mkazi wa Tanganyika amesema zamani wazazi walikuwa na utamaduni wa kukutana na watoto wao ndiyo maana hapakuwa na matendo ya unyang'anyi, kuporomoka kwa maadili tofauti na sasa ambapo wazazi hawana muda wa kuzungumza na watoto zaidi wanarudi usiku.
MWISHO.
Monday, 8 May 2023
WILAYA YA TANGANYIKA: YAWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KWA AJILI YA KILIMO NA MIFUGO.
HAYO yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mheshimiwa Onesmo Buswelu alipoitembelea kampuni ya Meru Agro Wilayani Mbozi akiwa pamoja na kamati ya ulinzi ya Wilaya, Waheshimiwa Madiwani na Wakuu wa Idara.
Friday, 28 April 2023
TANGANYIKA MUUNGANO CUP YATAMATIKA KWA MAJALILA FC KUIBUKA MSHINDI.
MKUU wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu leo Aprili 27,2023 amehitimisha mashindano ya Muungano CUP yaliyokuwa yanalindima wilayani humo kwa kukabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi.
Timu ya Majalila FC imeibuka mshindi wa kwanza wa mashindano hayo, katika fainali iliyochezwa katika Uwanja wa michezo Majalila shule ya msingi kwa kuitandika Sijonga FC bao mbili kwa bila.
Akihutubia wakazi wa mji wa Majalila mara baada ya kumalizika kwa fainali kati ya Majalila FC dhidi ya Sijonga FC, DC Buswelu amewapongeza washiriki wote wa mashindano hayo, kwani ni njia moja wapo ya kudumisha mshikamano kama ilivyo asisiwa na waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere na Hayati Abeid Karume.
DC Buswelu amesema kutokana na jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika michezo, Serikali wilayani Tanganyika imekusudia katika bajeti yake ya Mwaka wa fedha huu kutenga fedha kwa ajili ya kujenga Uwanja wa kisasa wa mpira.
Kwa upande wake Kaimu mkuu kitengo cha michezo Halmashauri ya Tanganyika, Otuman Kasamya amesema katika mashindano hayo mshindi wa kwanza ambaye ni Majalila FC amepata zawadi ya shilingi elfu Themanini na kikombe, mshindi wa Pili shilingi elfu Hamsini, mshindi wa Tatu shilingi elfu 30 huku mshindi wa Insha akijipatia zawadi ya shilingi elfu Ishirini ambaye ni mwanafunzi kutoka Kakoso Sekondari na mwamuzi bora aliyejioatia shilingi elfu Ishirini.
MWISHO.
MKUU WA WILAYA YA TANGANYIKA AWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA AFYA BULAMATA.
"Leo tunawapa vyandarua tunaomba mkavitumie kujikinga na Malaria. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hataki kuona mwananchi wake anapoteza maisha kwa sababu ya Malaria ndiyo maana ameleta vyandarua na Madaktari"
Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu (kulia) akifuarahi na Diwani wa Kata ya Bulamata baada ya kuweka Jiwe la Msingi kituo cha Afya Bulamata.
Mkuu wa wilaya akimkabidhi chandarua mama mjamzito kama sehemu ya Serikali kuwakinga Wananchi wake dhidi ya Malaria.
Awali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Tanganyika, Dkt. Alex Mrema alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa Serikali imeleta vifaa kwa ajili ya mama wajawazito ikiwemo vyandarua ambavyo vitakawiwa bure.
Baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma katika kituo hicho wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea kituo cha Afya karibu kwani mwanzo walikuwa napata shida kufuata huduma maeneo ya mbali.
MWISHO.
WANANCHI TANGANYIKA WAADHIMISHA MUUNGANO KWA KUIISHUKURU SERIKALI.
WANANCHI wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi wameadhimisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Vikonge hadi Uvinza mkoani Kigoma kwa kiwango cha lami.
Wakizungumza mbele ya msafara wa mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu aliyeambatana na viongozi wengine walipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Vikonge - Luhafwe (km 25) Aprili 25,2023 walisema kabla ya Uhuru walilazimika kukatiza maporini kufuata huduma za Afya jambo lililosababisha vifo kwa Mama wajawazito.
"Tulipata shida sana, unakuta mama mjamzito anatoka mbali wanapopatwa na uchungu mtu anazalia njiani, kiti (mtoto) kinakataa kutoka mtu anafariki" Alisema Devotha Titto mkazi wa Kijiji cha Vikonge.
Alisema mbali na kuwarahisishia usafiri lakini pia anaimani hata kiwango cha nauli kitakuwa chini ikiwemo ufupi wa safari kutoka Mpanda hadi Kigoma kwani kwa sasa wanatumia hadi masaa Sita kufika mkoani Kigoma.
Diwani wa Kata ya Tongwe Frank Kidigasi alisema kukamilika kwa barabara hiyo ya Mpanda - Kigoma itafungua fursa kwa wakazi wa Tanganyika na Katavi kwa ujumla kufanya biashara Kigoma na nchi jirani za Congo, Rwanda na Burundi kwa kuuza mazao yao kwa kuwa mkoa wa Katavi ni wa Kilimo.
Diwani wa Kata ya Tongwe Frank Kidigasi
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji mradi huo, Kaimu Meneja Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Katavi Mhanfisi Emily Zengo alisema barabara hiyo inajengwa kwa fedha za ndani kwa ghalama ya Tsh. bilioni 35.638.
Alisema, kazi inayofanyika ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kukata sehemu ambazo milima iko juu sana, ujenzi wa daraja kubwa Mnyamasi lenye urefu wa mita 61.8 na kina cha mita 5 ambalo litakuwa suluhisho eneo hilo kwa kuwa mvua zinaponyesha maji yanapita juu ya barabara.
Kaimu Meneja Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Katavi Mhanfisi Emily Zengo.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu alisema ziara hiyo ni kuadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo amemhakikishia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Serikali ya Tanganyika itasimamia miradi yote kwa ufanisi ili Wananchi waweze kupata thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu akifurahia na Wananchi baada ya kutembelea mradi wa barabara katika maadhimisho ya sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
MWISHO.
Thursday, 6 April 2023
TANGANYIKA: KISHINDO CHA SERIKALI YA AWAMU YA SITA NDANI YA MIAKA MIWILI YA UONGOZI WA RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN.
ZAIDI ya shilingi Bilioni 131 zimekusanywa, kupokelewa na kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-25 katika Wilaya hiyo kwa kipindi cha miaka miwili( Machi 2021- 2023 ) cha serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameyasema hayo katika kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Tanganyika kilichoketi Jana Aprili 5, 2023 katika ukumbi wa Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani humo.
DC Buswelu amesema fedha hizo shilingi 131,791,925,200.5 zimefanikisha kuifungua Tanganyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo Afya, barabara, kilimo, elimu, maji, mawasiliano na uchukuzi, umeme vijijini, uwekezaji sanjari na sekta mbalimbali.
Katika sekta ya Afya ndani ya miaka miwili, wilaya hiyo ilipokea zaidi ya bilioni 4 ambazo zimetumika katika ujenzi wa miundombinu ya Afya kama ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi na ujenzi wa wodi tatu katika hospitali ya wilaya ya Tanganyika ikiwemo ujenzi wa vituo vya Afya, Zahanati na vyumba za watumishi.
Amesema, katika sekta ya barabara Wilaya ya Tanganyika sasa imeunganishwa na mtandao wa barabara hali inayochochea uwekezaji ikiwemo wananchi kujiingizia kipato kupitia usafiri na usafirishaji.
"Ujenzi wa barabara ya Vikonge - Luhafye yenye urefu wa KM 25 inayojengwa kwa fedha za kitanzania zaidi ya bilioni 35 mkandarasi yupo eneo la mradi na ujenzi unaendelea, barabara ya Kagwira - Ikola - Karema yenye urefu wa KM 120 ipo hatua ya awali ya upembuzi ambayo imefikia asilimia 95 na kiasi cha shilingi bilioni 1.073 kimetolewa" Alisema Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanganyika Yasin Kiberiti akifuatilia taarifa ya utekelezaji wa Ilani ikisomwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika
Baadhi ya Wajumbe wakifuatilia hotu ikisomwa kuhusu hatua ambayo Wilaya ya Tanganyika imepiga ndani ya kipindi cha miaka Miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan
Barabara nyingine zinazotengenezwa chini ya TANROAD ni ya Kibo - Mwese - Lugonesi, Kagwira - Karema na Mpanda - Uvinza huku Wakala wa mjini na vijijini TARURA akiongezewa bajeti kutoka 641,150,000 mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia 4,157,455,928.18 kwa mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 259.
Aidha, amesema sekta ya elimu imeimarika mara dufu baada ya kujengwa miundombinu ya kutosha ambapo kupitia fedha za UVIKO-19 jumla ya vyumba vya madarasa 196 vimejengwa ( shule ya msingi vyumba 127 na shule za Sekondari vyumba 69) na kupitia fedha za mapato ya ndani na hewa ukaa jumla ya vyumba 94 vimejengwa ikiwemo kujenga shule mpya ya Majalila, mabweni n.k
Pia chuo cha ufundi stadi (VETA) ujenzi wake unatarajia kuanza mwezi huu eneo la Kijiji cha Majalila.
Maeneo mengine aliyoyata wilaya hiyo kupiga hatua ni sekta ya maji ambapo shilingi 6,481,086,307.46 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji ambapo miradi 15 itakayonufaisha vijiji 22 inajengwa na baadhi imeanza kutoa huduma.
Hata hivyo, amesema sekta ya maliasili na utalii imezidi kuimarika ambapo kutokana na utunzaji na usimamizi mzuri wa maliasili na misitu, jumla ya vijiji 8 vya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika vimenufaika na mradi wa hewa ukaa ambapo shilingi bilioni 6.57 zimepatikana ndani ya miaka miwili.
Fedha hizo zimetumika kujenga madarasa, zahanati, kuajiri walimu wa mikataba, kutoa vyakula kwa wanafunzi shuleni, kuajiri Askari walinzi wa misitu na kukopesha vikundi vya wajasiriamali vijijini kupitia COCOBA.
Wilaya ya Tanganyika ilianzishwa mwaka 2016 ikijulikana wilaya ya Mpanda Vijijini ambapo jina la Tanganyika lilitokana na Ziwa Tanganyika lililopo kwenye mpaka wa mashariki ya eneo hili.
Katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, idadi ya wakazi wa wilaya ni 371836.
MWISHO.