Sunday, 12 February 2023

RC MRINDOKO AKOSHWA NA MRADI ULIOTEKELEZWA KWA FEDHA ZA HEWA UKAA.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akizungumza na Wananchi pamoja na wanafunzi baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali Halmashauri ya Tanganyika.

MKUU wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa Ujenzi wa nyumba ya Walimu yenye uwezo wa kubeba watumishi wawili iliyojengwa kwa Fedha za hewa ukaa katika Kijiji cha Lwega Kata ya Mwese Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Februari 10, 2023 katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani Tanganyika Mkuu wa Mkoa Mrindoko amewapongeza Viongozi wa Kata na Vijiji pamoja na kamati mbalimbali za ujenzi kwa kufanikisha Ujenzi wa Jengo hilo ambalo  hadi sasa limegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 94.
Nyumba ya walimu (Two in One) inayojengwa katika Kijiji cha Lwega Kata ya Mwese Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kupitia fedha za mradi wa hewa ukaa. Mradi huu umefikia hatua ya umaliziaji.

Mhe Mrindoko amehimiza Walimu kutimiza wajibu wao kikamilifu Shuleni hapo kwa kuwa Serikali imetimiza wajivu wake kikamilifu katika kujenga mazingara wezeshi kwa wao kufanya kazi shuleni hapo.

Aidha amewataka Wananchi kutosikiliza kelele kuhusu miradi inayotekelezwa kwa fedha za hewa ukaa na badala yake waelekeze jitihada zaidi katika utunzaji wa misitu kusudi waweze kunufaika zaidi na matunda ya utunzaji wa Misitu Kijijini hapo.

Miradi mingine inayotekelezwa kwa fedha zitokanazo na mapato ya hewa ukaa baadhi yake ni pamoja na Zahanati ya Lugonesi, Zahanati ya Mpembe, Vyumba vya madarasa, Nyumba za walimu Kijiji cha Lwega na jengo la utawala Shule ya Sekondari Mwese.


Picha ya 1,2 na 3 ni mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Zahanati ya Lugonesi iliyofikia hatua ya upigaji ripu na Zahanati ya Lugonesi ambayo imefikia asilimia 90 na miradi inajengwa kwa fedha za hewa ukaa.

Mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Mpembe Kata ya Katuma unaotekelezwa kupitia fedha za mradi wa hewa ukaa.


Vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwa fedha zitokanazo na fedha za mradi wa hewa ukaa.
Mradi wa ujenzi Jengo la utawala Shule ya Sekondari Mwese kupitia fedha za hewa ukaa,ujenzi wake umekamilika.
Mradi wa ujenzi Ofisi ya Kijiji Lwega, mradi umejengwa kwa fedha za hewa ukaa.

Saturday, 11 February 2023

CCM TANGANYIKA YAAHIDI USHIRIKIANO KUFIKIA MALENGO YA KUKUSANYA BILIONI 40.3

MWENYEKITI wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi Yasin Kiberiti amesema hana wasiwasi na halmashauri ya Tanganyika kufikia na hata kuzidi lengo la kukusanya na kutumia Tsh. Bilioni 40.3 endapo vyanzo vya mapato vitasimamiwa vizuri.

Ameyasema hayo katika kikao cha baraza maalumu la madiwani la kupitia na kujadili rasimu ya bajeti ya mwaka 2023/24, kikao kilichofanyika Jana Februari 10, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Mkurugenzi.

"Na sisi tutakutana na wenzetu Ofisi ya Mkuu wa wilaya kwa maana ya kusimamia bajeti kuhakikisha mapato yote tuliyojiwekea, mamilioni haya tuliyojiwekea yanakamilika lakini yanazidi hizo asilimia. Tukisimamia vizuri naamini hizo zitazidi"

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi Yasin Kiberiti.

Naye Katibu Tawala wilaya ya Tanganyika Geofrey Mwashitete amesema ili kufikia malengo hayo wataandaa mazingira mazuri kwa mamlaka za Serikali za mitaa ikiwemo kutoa ushirikiano.

"Kwa kweli inaonekana ni bajeti nzuri na kubwa kwa sababu kama mwaka huu mapato ya ndani imepangwa Bilioni 10 na milioni 12 ikilinganishwa na mwaka jana tulikuwa kwenye Bilioni tano na kidogo kwa hiyo tumepaa na tafsili yake ni kwamba mambo mengi yatatekelezwa"

Katibu Tawala wilaya ya Tanganyika Geofrey Mwashitete.

Akihitimisha kikao hicho Mwenyekiti wa halmashauri ya Tanganyika Hamad Mapengo amewashukuru madiwani kwa michango yao pamoja kuipitisha rasimu ya bajeti ya mwaka 2023/24 iliyowasilishwa na Afisa mipango wilaya ya Tanganyika Deus Luziga.

Aidha, amesema mapendekezo yote yaliyopendekezwa ikiwemo kuongeza vyanzo vya mapato vitazingatiwa kwa kuwa vitaiongezea halmashauri mapato jambo litakalowezesha kutekeleza miradi mbalimbali hadi ya ziada.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Tanganyika Hamad Mapengo.




Sehemu ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho.

MWISHO.

Wednesday, 8 February 2023

HALMASHAURI YA TANGANYIKA KUKUSANYA TSH. BILIONI 40.3 MWAKA WA FEDHA 2023/24.

PICHA: Kushoto ni Mwenyekiti wa Kikao cha kamati ya ushauri Wilaya (DCC) Wilaya ya Tanganyika ambaye pia ni mkuu wa wilaya Onesmo Buswelu akiteta jambo na Mkurugenzi mtendaji Juma Shabani (mwenye miwani) pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tanganyika Hamad Mapengo.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 inatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha Tsh. Bilioni 40.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.5 ya bajeti ya mwaka 2022/23 ya Tsh. Bilioni 32.6

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tanganyika Juma Shaban leo Februari 8, 2023 alipokuwa akiwasilisha taarifa ya rasimu ya bajeti mbele ya wajumbe katika Kikao cha kamati ya ushauri Wilaya (DCC) Wilaya ya Tanganyika kilichoongozwa na mwenyekiti wake ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkurugenzi.

Mkurugenzi huyo amesema chanzo cha bajeti hiyo kuongezeka ni kutokana na kuongezeka kwa makisio ya mishahara ya Watumishi, vyanzo vya mapato hasa chanzo cha mrahaba unaotokana na hewa ukaa, uuzaji wa Viwanja, kuongezeka kwa mazao ya kilimo na kutokana na kukua kwa biashara ya mazao ndani na nje ya Nchi.

Amesema Halmashauri hiyo imepanga kukusanya kiasi hicho cha fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo mapato ya ndani, fedha za ruzuku kutoka Serikali kuu na ruzuku kutoka kwa wafadhili na wahisani.

"Kwanza tuna mapato ya ndani ambayo yana jumla ya Bilioni 10 ambayo bajeti hii imeongezeka ukilinganisha na bajeti ya mwaka uliopita, kutokana na kuongezeka kwa bajeti matumizi mengineyo ni asilimia 40 na miradi ya maendeleo itakuwa asilimia 60"

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tanganyika Juma Shaban akiwasilisha mpango wa rasimu ya bajeti kwa Mwaka wa fedha 2023/24 katika kikao cha DCC kilichofanyika leo katika Ukumbi wa mikutano wa Mkurugenzi.

Aidha ameongeza kuwa "kuna chanzo ambacho ni fedha za hewa ukaa ambazo hizi ni mapato fungiwa kwa sababu fedha hizi zinaenda moja kwa moja kwenye Vijiji husika ambapo imekadiriwa kupokea Bilioni Nne na Milioni mia mbili na kumi na mbili elfu"

Amesema bajeti hiyo imezingatia kukamilisha ujenzi wa miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ikiwemo kuimarisha sekta ya afya, elimu na Maliasili.

Mikakati mingine ni kujenga shule ya mchepuo wa kingereza (English medium) ili kutatua tatizo la aina hiyo ya shule katika Halmashauri, kuboresha kituo cha Afya Sibwesa kuwa cha mfano, kuboresha Hospitali ya Ikola na kuanzisha kituo cha nyuki cha kuchataka asali sambamba na kukarabati nyumba zipatazo 14 za Halmashauri zilizopo Mpanda mjini ukiwemo ukumbi wa Idara ya Maji.

Katika sekata ya Maji akiwasilisha rasimu ya bajeti Mhandisi wa Wakala wa Usambazaji wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Tanganyika Festo Mpogole amesema katika mwaka wa fedha 2023/24 RUWASA wilayani Tanganyika imepanga kutumia Tsh. Bilioni 1.6 kutekeleza miradi mbalimbali ya maji.

Nae mwakilishi kutoka Wakala wa Barabara za mijini na vijijini (TARURA) wilaya ya Tanganyika Mhandisi Bonventure Katambi amesema jumla ya Tsh. Bilioni 4.7 zinatarajiwa kutumika katika matengenezo ya barabara wilayani humo.


PICHA ya kwanza ni Mhandisi wa Wakala wa Usambazaji wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Tanganyika Festo Mpogole na Picha ya pili ni Mhandisi Bonventure Katambi kutoka Wakala wa Barabara za mijini na vijijini (TARURA) wilaya ya Tanganyika wakiwasilisha taarifa.

Akihitimisha Kikao hicho, Mwenyekiti wa kikao ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amehimiza kupanga mipango mathubuti ya ukusanyaji mapato ili kufikia adhima ya utekelezaji wa miradi.

Aidha, ametumia kikao hicho kutoa wito kwa Watumishi kutimiza wajibu wao kwa kuchapa kazi na kuzingatia ufanisi huku akiwaomba Viongozi wa Dini kuwaombea Viongozi ili waweze kutimiza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.

Mwenyekiti wa Kikao cha kamati ya ushauri Wilaya (DCC) Wilaya ya Tanganyika  ambaye pia ni mkuu wa wilaya Onesmo Buswelu akitoa maelekezo wakati akifunga kikao.

Rasmu hiyo ya bajeti inatarajiwa kusomwa na kupitishwa katika kikao cha bajeti cha baraza la madiwani siku ya Ijumaa tarehe 10 Februari 2023.










Picha mbalimbali zikiwaonyesha wajumbe waliohudhuria kikao Kikao cha kamati ya ushauri Wilaya (DCC) Wilaya ya Tanganyika

MWISHO.

Sunday, 5 February 2023

RC KATAVI ATAJA MAFANIKIO YA MKOA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 46 YA CCM.

MKUU wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema kwa kipindi cha Miaka miwili na nusu chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoa na taasisi zake umetumia zaidi ya Tsh. Bilioni 620 katika kutekeleza miradi mbalimbali.

Mhe. Mrindoko amesema katika sekta ya elimu mkoa umepata vyumba vya madarasa 119 katika shule za sekondari na kuwezesha wanafunzi 14,854 waliofaulu kidato cha kwanza kuweza kupata Sehemu ya kusomea.

Amesema sekta ya afya mkoa wa Katavi umepata Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambayo imeanza kutoa huduma, Hospitali 5 za wilaya, vituo vya Afya zaidi ya 14 na Zahanati zaidi ya 20 ambapo miradi hiyo yote imetekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani, Serikali kuu na zingine kutoka kwa wafadhili na wadau mbalimbali.

Mhe. Mrindoko ametaja mafanikio mengine ya chama cha mapinduzi katika sekta ya maji kuwa mkoa wa Katavi umefikia asilimia 70.7 ya upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 60 mjini huku Mpanda mjini ikitarajia kufikisha asilimia 100 ya upatikanaji wa maji kupitia mradi wa "miji 28" unaotarajia kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha.

Kadhalika RC Mrindoko amesema katika sekta ya miundombinu yapo mafanikio makubwa ikiwemo mkoa kuunganishwa na mikoa mbalimbali kwa kiwango cha lami na kiasi cha Tsh. Bilioni 4 kinatarajiwa kutumika kukarabati barabara za miji na vijijini kupitia TARURA ikiwemo ujenzi wa madaraja makubwa likiwemo daraja la Mto Msadya na daraja la Ifinsi.

"Mheshimiwa mwenyekiti kama ulivyotuagiza barabara hii ya inayoingia eneo la Kabatini ni barabara ambayo ina hali mbaya, nikuhakikishie barabara hii imetengewa Milioni 200 katika mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai 2023 barabara hii itaweza kufanyiwa matengenezo"


Mafanikio mengine ni kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo migogoro 74 ambayo ipo kwenye timu ya Mawaziri nane imeweza kuwasilishwa na migogoro hiyo ipo katika hatua za mwisho za utatuzi.

Aidha, aametoa wito kwa wananchi kutunza Misitu.


Baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kuadhimisha Miaka 46 ya CCM katika viwanja vya Shule ya Msingi Kabatini leo Februari 5,2023.

MWISHO.

UJUMBE WA CCM MKOA WA KATAVI KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 46.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi Comred Idd Kimanta,mgeni rasmi katika maadhimisho ya Miaka 46 ya CCM.

Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi Comrade Idd Kimanta amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho mkoani Katavi kuacha majungu badala yake watengeneze mahusiano mazuri na Watumishi kwa kuwa wao ndio watekelezaji wa Ilani.

Kimanta ametoa kauli hiyo leo akiwa Kijiji cha Mpembe kitongoji cha Kabatini halmashauri ya wilaya ya Tanganyika akihutubia Wananchi wa kitongoji hicho katika kelele cha maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa chama hicho.

Amesema kamati ya siasa mkoani humo haitasita kumchukulia hatua Kiongozi wa chama ambaye atabainika kuvuruga mahusiano baina ya Serikali na chama hali kadhalika kwa Mtumishi atakayebainika kuvuruga mahusiano baina ya chama na Serikali.

"Sisi wote ni Binadamu kukitokea kutoelewana basi kutoelewana huko kuzungumzwe kwa kuheshimiana, hatutarajii tufike mahali tukute Kiongozi wa chama au Kiongozi wa Serikali anamdharau mwenzake"

Amesema pamoja na kuisimamia Serikali lazima chama hicho kiilinde kwa kuiunga mkono huku akimtaka Mkuu wa mkoa huo kuwachukulia hatua Watumishi wote wazembe wanaokwamisha maendeleo ya Mkoa na ilani ya chama.

"Kwenye tenga samaki mmoja akioza toa yule aliyeoza halafu wale wengine waendelee wawe kitoweo. Mtumishi mmoja asiharibu sifa ya Watumishi wengine, toa yule wengine wazuri tunaendelea kuwa nao hakuna cha samaki mmoja akioza wote wameoza"

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi Comred Idd Kimanta akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko.

Aidha, ametoa wito kwa wana CCM kutambua wajibu wao na kufanya ziara kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua huku akiwasihii Watanzania kuendelea kuwa na imani na chama cha mapinduzi kwa kuwa ndicho chama pekee kinachoweza kutatua kero zao.

"Chama kinapokwenda ndani ya wananchi kinasikia nini wananchi wanataka. Chama lazima kila siku kisikie wananchi wanataka nini kwa sababu chama ndio kimbilio la wananchi"

Pamoja na yote, chama cha (CCM) Mkoa wa Katavi kimehitimisha maadhimisho hayo kwa kuwakabidhi kadi za uanachama wanachama wapya 2700.

Chama cha Mapinduzi (CCM) leo Februari 5,2023 kinaadhimisha Miaka 46 toka kuanzishwa kwake Februari 5, 1977.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi Comred Idd Kimanta akikabidhi kadi kwa mmoja wa wanachama wapya.





Thursday, 2 February 2023

MWENYEKITI CCM WILAYA YA TANGANYIKA: WATENDAJI TIMIZENI WAJIBU WENU.


Pichani ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanganyika Ndg. Yasin Kiberiti iliyochukuliwa wakati wa ziara.

Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi imesema wajumbe wanapofanya ziara ya kukagua miradi ni kutaka kujiridhisha utendaji kazi wa Watumishi na usahihi wa matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama hicho wilaya ya Tanganyika Yasin Kiberiti katika kikao cha majumuisho baada ya ziara ya siku Tano katika Kata 14 iliyofanywa na kamati hiyo kumalizika.

Kiberiti amesema katika ziara hiyo wamebaini wapo baadhi ya watumishi hawakai kwenye vituo vyao vya kazi na wengine wapo lakini hawatekelezi wajibu wao wa kuwatumikia wananchi.

Aidha, kamati imebaini ubadhilifu wa wizi wa vifaa vya ujenzi ambapo katika baadhi ya miradi wamekuta ndoo nne za rangi zimeibwa.

"Wapo baadhi ya Watumishi walioko huko chini hawakai kwenye vituo vyao, hilo tumeshalibaini tunalo. Kuna baadhi ya Watumishi hawatekelezi wajibu wao maana yupo kama Mwananchi wa kawaida na kila kinachofanyika yeye hajui"

Amesema watu wa namna hiyo wanaweza kumsababishia Mkurugenzi Mtendaji  shida kwa kuwa usimamizi wao kwenye miradi ya Maendeleo ni hafifu.

Akiwasilisha mapendekezo ya kamati katika baadhi ya miradi waliyotembelea Katibu wa CCM wilaya ya Tanganyika Ndugu Adelaida Paskal Machenchewa amesema kamati imependekeza fedha itafutwe popote ili kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kapemba na iweze kutoa huduma zinazostahili kutolewa.

Pia kamati imependekeza kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo Mradi wa maji vijiji vya Isenga, Ifumbura na Kapemba unaoghalimu zaidi ya Tsh. Bilioni 1.3 ambapo mradi umefikia asilimia 60 na mradi unapaswa kukamilika Machi 30,2023 sambamba na miradi mingine.

Pamoja na hayo, kamati imeipongeza Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hssan kwa kutenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bweni la wanafunzi shule ya sekondari Kabungu wenye thamani ya zaidi ya Tsh. Milioni 69.

"Kamati ya siasa ya  chama cha Mapinduzi licha ya kupongeza, iliomba na kuagiza wanafunzi wote waliotakiwa kuripoti katika shule ya sekondari Kabungu waripoti"

MWISHO

HALMASHAURI YA TANGANYIKA YAWEKA MIKAKATI KUONGEZA VYANZO VYA MAPATO.


HALMASHAURI ya wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi katika kuongeza vyanzo vya mapato inakusudia katika bajeti ijayo kutenga fedha kwa ajili ya kujenga uwanja wa mpira ili kupitia mashindano mbalimbali halmashauri hiyo iweze kujiingizia mapato.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Shaban Juma, wakati akijibu hoja ya Diwani wa Kata ya Tongwe Frank Kibigasi katika kikao cha kawaida cha Baraza la madiwani aliyetaka kujua mikakati ya halmashauri katika kubuni chanzo cha mapato kupitia michezo na kusema kuwa tayari ameshampatia maelekezo Afisa Utamaduni kutafuta eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa.

"Katika dunia ya leo sehemu nyingi masuala ya michezo wanayapa umuhimu ila sisi wilayani hapa hatuna kiwanja cha michezo. Tunaangalia eneo zuri ambalo linaweza kuwa kubwa na linafikika na watu kwa ukaribu ili tuweze kuingiza nguvu zetu"

Aidha, Diwani Kibigasi ameishauri halmashauri kuanzisha kituo cha kukusanyia ushuru eneo la Ngomalusambo kwa kuwa eneo hilo mazao yanapitishwa kiholela jambo linaloikosesha halmashauri mapato na kuinufaisha halmashauri nyingine.


Diwani wa Kata ya Tongwe Frank Kibigasi akichangia hoja katika taarifa ya kamati ya fedha kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la madiwani Tarehe 2,2,2023 katika Ukumbi wa mikutano wa Mkurugenzi.

Akichangia hoja hiyo, Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesema kipaumbele cha kwanza cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mapato hivyo halmashauri inapaswa kujipanga kutokana na mahitaji kuongezeka kila leo.


Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Hamad Mapengo amemtaka mkurugenzi kufanyia kazi ushauri uliotolewa na wajumbe wa Baralaza hilo ili kuleta ufanisi katika eneo la ukusanyaji mapato.

Katika hatua nyingine, Mapengo amewaomba Madiwani kuisaidia Serikali kuhimiza watoto waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza kuripoti haraka Shuleni.

"Turudi kwenye Kata zetu tuwahimize watendaji wa Vijiji. Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi sana za kukamilisha miundombinu ya ujenzi wa madarasa,nyumba za walimu, tumepata fedha za madawati mmeona na Watumishi wanaendelea kufika kwa hiyo kazi yetu ni kuhakikisha tunahimiza wale watoto waende wakaripoti" alisema Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mhe. Hamad Mapengo.

Katika shule ya Sekondari Majalila wanafunzi wapatao 27 bado hawajaripoti hadi sasa licha ya masomo kuanza jambo ambalo Mkuu wa wilaya ameagiza wanafunzi hao wabainishwe na wasakwe ili wakajiunge na masomo.